OFISI YA MSAJILI WA HAZINA YAKUSANYA SH.BILLIONI 852.9 SAWA NA ASILIMIA 109.5 YA LENGO

 📌RHODA SIMBA

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema katika mwaka wa fedha 2021/22 imekusanya sh.bilioni 852.9 sawa na asilimia 109.5 ya lengo ambapo lengo lilikuwa kukusanya sh.Bilioni 779.03 sawa na asilimia 33.5.

Hii ni zaidi ya kiasi kilichokusanywa tarehe 30 Juni mwaka 2021 ambacho kilikuwa ni sh.Bilioni 638.87.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa uwekezaji Ofisi ya Msajili wa Hazina Lightness Mauki wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa Ofisi hiyo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema mapato hayo yamekusanywa kutoka katika mapato yasiyo na kodi ambayo yanajumuisha gawio, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi na mapato mengineyo.

Kadhalika amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea na juhudi za kusimamia utendaji wa kampuni ambazo Serikali inaumiliki wa hisa chache ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano na wabia wenza na kusimamia kwa ukaribu matumizi yasiyo ya lazima ambapo ongezeko la gawio kwa wanahisa limeonekana.

Mathalani mafanikio ya jitihada hizo yamejidhihirisha katika utendaji wa Banki ya NBC ambayo imeongeza faida kabla ya Kodi kutoka sh.bilioni 7 mwaka 2020 hadi sh.bilioni 60 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57, ukuaji huu wa faida umewezesha benki hii kutoa gawio kwa Serikali sh. Bilioni 4.5 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa

 Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeanzishwa kupitia sheria ya msajili wa Hazina (mamlaka na majukumu) sura 370 lengo kuu la kuanzishwa kwa OMH ni kusimamia uwekezaji na Mali zingine za Serikali katika Taasisi na mashirika ya umma, pamoja na kampuni ambazo Serikali inaumiliki wa hisa au kuna maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwaajili ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments