SERIKALI YAAGIZA TSC KUWACHUKULIA HATUA WALIMU

 ðŸ“Œ JASMINE SHAMWEPU

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais Tamisemi, imeitaka Tume ya Utumishi wa Walimu nchini TSC kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya walimu ambao wamekuwa wakifanya vitendo viovu ambavyo ni kinyume na maadili ya taaluma yao huku akiagiza Tume hiyo kuangalia changamoto inayo sababisha kuongezeka kwa utoro kwa Walimu nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI anayeshugulikia Afya, Festo Ndugange ametoa maagizo hayo hii leo Jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu TSC.

Kumekuwa na tatizo la utovu wa nidhamu kwa Walimu ni muhimu Viongozi wa Tume kuchukua hatua kwa baadhi ya walimu

Ndugange

Aidha amesema kunahitajika kuchukua hatua kutokana na kosa la utoro kuongezeka kwa uzito mkubwa sawa na asilimia 66.

Ndugange amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali watumishi hasa Walimu ambapo imeweza kuwapandisha vyeo zaidi ya Walimu laki mbili kwa mwaka 2021/2022 ikiwa ni pamoja na kulipa stahili mbalimbali za madai ambapo amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti katika kada hiyo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kwa upande wake Katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo, Paulina Nkwama ameishukuru Serikali kwa kushughulikia madai mbalimbali na kueleza mashauri ya walimu ambayo wameyashughulikia.

Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Walimu nchini TSC limekutana kwa lengo la kujadili Kuhusu wajibu na Haki za wafanyakazi ikiwemo hoja mbalimbali za wajumbe zitakazowasilishwa kutoka katika kila Kanda.

 

Post a Comment

0 Comments