TSC YAWATAKA WALIMU KUENDELEA KUZINGATIA MIIKO NA MAADILI YA KAZI ZAO

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA 

ILI kuongeza tija ya ufundishaji Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)  imewataka walimu kuzingatia miiko na maadili ya kazi zao na  kutekeleza majukumu kwa weledi  ili  kuleta ubora wa elimu hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa TSC Mwalimu Paulina Mkwama wakati akizungumza na waandishi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo.

Amesema, chombo hicho kimekuwa kikitoa elimu kwa walimu ili wafanye kazi yao kwa kuzingatia maadili huku akisema pamoja na jitihada hizo lakini bado kuna walimu ambao wamekuwa hawazingatii miiko na maadili ya kazi yao.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, walimu hao wasiozingatia maadili ya kazi yao huilazimu TSC kuwafikisha kwenye mamlaka zao za nidhamu kwa mujibu wa kanuni kwa ajili ya kushughulikiwa kwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili kuwanusuru watoto na kuwafanya wapate huduma iliyokusudiwa.

Tume hii imejikita zaidi katika elimu kwa walimu ili watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ambapo watendaji wa Wilaya wamekuwa wakifika shuleni kutoa elimu kwa walimu kuhusu ajira na maendeleo ya walimu pamoja na maadili na kujiepusha na makosa ya kinidhamu kwa walimu.

Mwalimu Mkwama

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa elimu kwa watoto hapa nchini huku akiwasihi kwamba TSC ipo pamoja nao kuhakikisha walimu wanapata stahiki zao .

Naomba nisisitize kuwa TSC ni chombo chenu kimeundwa kuwahudumia, hakipo kwa ajili ya kuwafukuza kazi walimu la hasha, bali kimeundwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kuwahudumia walimu katika ajira zao, maadli ya utumishi wao kwa kuhakikisha kwamba walimu wanafanya kazi zao kwa kuzingatia miiko ya maadili ya kazi ya ualimu na maendeleo yao katika utumishi wa umma

Mwalimu Mkwama.

 

Post a Comment

0 Comments