UMASKINI WA FAMILIA UNAVYOCHOCHEA NDOA ZA UTOTONI.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA DODOMA

Tina Aloyce (si jina lake halisi), kutoka kijiji cha Ngwenda Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma ni msichana aliyeozeshwa akiwa na umri wa miaka 15 tu, anasema hakuwa na maamuzi, wazazi wake waliamua kumuozesha akiwa na umri huo ili fedha ya mahari itakayopatikana iweze kuhudumia familia nyumbani.

“Mimi niliishia darasa la tano tu, maisha nyumbani yalikuwa magumu sana, kuna muda nilikuwa nakosa mahitaji ya shule kama vile sare, vitabu nk.  Hapo ndipo nilipoona hakuna haja ya mimi kuendelea na masomo nikaacha shule,” anaongea Tina huku akiwa ameshika tama machozi yakiwa yana mlengalenga.

Kwa mujibu wa mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni nchini TECMN umebainisha kuwa umasikini au hali duni ya kaya nyingi nchini, imekua inachangia ongezeko la ndoa za utotoni kwa wasichana chini ya miaka 18. 

TECMN inasema Mkoa wa Dodoma una kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.   Takwimu zinaonesha Dodoma ina asilimia 51 ya ndoa za utotoni kwa Tanzania.

Tina anasema chanzo cha yeye kuacha shule mpaka kufikia kuolewa katika umri huo mdogo ni hali duni ya familia yao.

“Nikaacha shule nikawa namsaidia mama shughuli zake za nyumbani za kilimo na biashara yake, mama alikuwa anauza pombe za kienyeji, akajitokeza mwanaume akasema anataka kunioa, baba na mama wakaridhia wakampangia mahari, akatoa akanioa,” anaelezea Tina kwa masikitiko.

HALI YA NDOA

Akizungumzia hali ya maisha yake baada ya ndoa anasema hakuwahi kufurahia ndoa hiyo alikuwa akipitia maisha magumu ya unyanyasaji   huku akisema hali ile anadhani ilikuwa inatokea kwasababu ya umri wake mdogo na kutokuwa na uelewa juu ya maisha.

“Nilikuwa napigwa, anakata fimbo nikifanya kosa hata liwe dogo tu ananichapa. Nikapata ujauzito, kujifungua kwangu kulikuwa kwa shida sana.  Kutokana na umri wangu mdogo, baada ya kujifungua manyanyaso yaliendelea ikabidi nitoroke na kurudi nyumbani kwa wazazi wangu.

“Mpaka sasa najutia, natamani ningesoma na mimi nipange maisha yangu kama watu wengine. Baada ya kurudi hapa nyumbani, nashukuru wazazi walinipokea. Siku hizi nafanya kazi ya mama lishe ambayo inanisaidia kuingiza kipato na kumhudumia mtoto wangu. Wito wangu kwa wasichana wenzangu, wasome na wazazi nao waache kutuozesha katika umri mdogo. Si unaona maisha nayoyapitia mimi?” anasema Tina, machozi yakimlengalenga. 

Ripoti ya tathmini ya mwaka 2018 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto- UNICEF inaonyesha kwamba huenda kukawa na ndoa nyingine za utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu.

Shirika hilo limeeleza kuwa takribani ndoa za utotoni milioni 25 zimezuiwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo kwa sasa, mtoto mmoja kati ya watano wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18 ukilinganisha na mmoja kati ya wanne aliyekuwa anaolewa kipindi hicho.

Aksa Masigazwa (Si jina halisi) ni msichana mwenye umri wa miaka 17 kutoka kijiji cha Nhinhi kilichopo Wilaya hiyo hiyo ya Chamwino, naye anasema chanzo cha kuolewa kwake ni tamaa ya wazazi kutaka kumiliki mifugo mingi kwa haraka.

“Mimi nilisoma mpaka darasa la saba nilivyomaliza tu, wazazi wangu wakaniambia niolewe na mtoto wa jirani yetu ambae alikuwa akimiliki mifugo mingi. Baba akachukua mahari ya ng’ombe, mbuzi na kondoo.  Nikaolewa.  Kwa kweli sikufurahia kuolewa.  Natamani na mimi ningeendelea na masomo kama wengine.  Ndoto yangu ndio iliishia pale, hapa nilipo mimi kwa sasa ni mkulima, nilitamani nami nisome nimalize niweze kupanga maisha yangu,”anasema Aksa.

UNICEF inasema kuwa mmoja kati ya watoto watatu wanapitia ndoa za utotoni kwa kipindi hiki Afrika ukilinganisha na mmoja kati ya watoto watano waliokuwa wakiolewa miaka kumi iliyopita.

WAZAZI WAFUNGUKA

Elias Matonya (si jina lake halisi) mkazi wa kijiji cha Nghwenda kilichopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma ni mzazi aliyewahi kumuozesha mtoto wake akiwa katika umri mdogo, anasema yeye hakuwa na uelewa ya kuwa mtoto wa kike pia anapaswa kusoma kama alivyo mtoto wa kiume.

“Maisha yetu hapa kijijini nilichokuwa naamini mtoto wa kike akiolewa anaweza wasaidia wenzake. Mimi nilimuozesha mtoto wangu akiwa na umri wa miaka 15. Hapa nyumbani nina watoto tisa, ile mahari ilinisaidia kuwahudumia wadogo zake mahitaji ya hapa nyumbani.

“Kumbe sikuwa nafahamu kwamba mtoto wa kike akisoma anaweza kuikomboa familia zaidi ya nilivyokuwa nafikiria, matokeo yake mtoto kawa ananyanyasika akarudi hapa nyumbani nikawa nawahudumia wote yani nikapata kazi mara mbili ya kulea watoto wawili,”anasema Matonya.

Julius Mhembano ambae naye hakutaka jina lake litajwe kutokana na sababu za kiusalama, ni mzazi pia aliyewahi kumuozesha binti yake akiwa katika umri mdogo, anasema yeye hakuwa na changamoto ila aliamini akimuozesha mtoto wake ataongeza mifugo.

“Mimi fahari yangu ilikuwa kuona zizi langu limejaa ng’ombe, mbuzi na kondoo. Niliwahi kuwaozesha watoto wangu wa kike watatu, mmoja alikuwa na miaka 14, wa pili miaka 13 na mwingine alikuwa na miaka 16, na kweli nilijaza zizi langu mifugo bila kujua kuwa nawakosesha watoto wangu haki za kusoma na kupanga maisha.

“Huwa najuta kuona watoto wa wenzangu wamesoma wana maisha mazuri mimi wangu wapo wanaishia kuteseka.  Natoa wito kwa wazazi wenzangu wasidanganyike. Wawapeleke watoto shule kwa sababu watoto wa kike pia wana haki,” anasema Mhembano. 

 WANAHARAKATI

Zakia Msangi ni mwanasheria kutoka shirika la wanawake linalotumia  sheria kumuokoa mwanamke na mtoto anayepitia ukatili wa kijinsia WILDAF. Anasema shirika lao muda mwingi limekuwa likipambana na masuala ya kupinga kwa kiasi kikubwa ndoa za utotoni kwa kutoa elimu kwa jamii kwa njia yamatamasha pamoja na vyombo vya habari, kwa kuzingatia sheria.

“Sheria ya mtoto ipo na imeeleza kabisa mtoto ni yule alie chini ya miaka 18 na haki za mtoto wajibu, lakini tunayo sheria ya ndoa ambayo inakinzana na kifungu hiki cha miaka 18 cha mtoto ambapo kifungu cha 13 na 17 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imeridhia mtoto wa kike aweze kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 na 14 kwa ridhaa ya mahakama. Sasa tunashangaa, sheria imemkubali mtoto ni chini ya miaka 18 sasa hii ya sheria bado inaruhusu mtoto wa miaka 15 aolewe sisi tunaendelea kuipigia kelele sheria hii kwa kutoa maoni.

“Tumeandika vifungu vyenye shida ikiwemo na hiyo ya ndoa na tumepeleka haya mapendekezo bungeni pamoja na Wizarani kuweza kupaka mabadiliko haraka iwezekanavyo” anasema Zakia

Anasema WILDAF imejikita katika sheria zaidi kwa sababu tayari ndoa za utotoni zipo na zinaendelea mtaani

“Tunaendelea kukemea kwa sababu madhara ni makubwa wanayoyapata watoto katika ndoa hizi za utotoni. Wengi hawapo tayari kiakili, kimwili na kimfumo kuweza kupokea majukumu mazito ya ndani ya ndoa. Watu wazima bado ndoa zinawashinda sembuse huyu mdogo ambaye anatakiwa acheze na watoto wenzie tayari tunamvika majukumu makubwa ya kulea familia wakati umri wake bado, tunakosea,” amesema Zakia.

Naomi Gerald ni Afisa Miradi kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali ya Rafiki Social Development Organization (RAFIKI SDO) iliyopo mkoani Shinyanga, Nayo imejikita katika masuala ya kupinga ndoa za utotoni, mimba za utotoni, afya pamoja na elimu. 

Naomi anasema mbinu moja wapo ya kupambana na hali hiyo ni kukutana na wazazi pamoja na mabinti wenyewe ili kuwapatia elimu.

“Kwa kiwango kikubwa sisi tunakutana na wazazi kupitia vijiwe mbalimbali ikiwemo vijiwe vya kahawa tunawapatia elimu kuhusu kupinga ndoa hizi za utotoni pia tunawaelimisha mabinti wenyewe, tunawapatia elimu pia ya masuala ya uzazi wa mpango akipata ile elimu basi hapati tena ile changamoto ambayo iliwahi mpata kwa wale ambao tayari wamepitia,” anasema.

“Tumefanikiwa kuwawezesha mabinti kwa kuwatengenezea vikundi vya kujikwamua kiuchumi ambavyo vinawakopesha nao wanafanya biashara ndogondogo ikiwemo kutengeneza sabuni, kupika karanga ili wajipatie kipato na hiyo inawaepusha na vishawishi ambavyo vinaweza kuwaingiza katika ndoa za utotoni,” anasema Naomi.

Anasema hizo kesi zipo na wanaendelea kutoa elimu kwa jamii huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika ambayo yanafanya harakati za kupinga ndoa hizi za utotoni.

“Jamii iwe tayari kufikiwa na kupata elimu kwa ajili ya kujikinga na masuala haya   ya ndoa za utotoni kwa sababu asilimia kubwa hali duni ya maisha katika familia inawafanya watoto wa kike waolewe mapema, akipata mwanaume ambae atakuwa anampatia pesa kidogo basi ni rahisi kuingia kwenye ndoa hizo ili mradi tu amhudumie hali duni aliyonayo,” anasema  Naomi.

Kuhusu muswaada wa kutaka kuongeza umri wa kuolewa kwa mtoto miaka 21 Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inasema inaendelea na zoezi la kukusanya na kuchambua maoni yakikamilika Wizara itawasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo ya ndoa.

Aidha kabla ya maamuzi hayo serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kutunga sheria mpya na kurekebisha sheria mbalimbali zinazohusiana na upingaji wa ukatili wa kijinsia na umri wa mtoto.

Sheria hizo ni pamoja na kutoa tafsiri ya mtoto katika sheria ya mikataba sura ya 345 kwa kuelezea umri sheria sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ambayo ilitoa tafsiri mtoto ni mwenye umri wa miaka 12 hadi 18 na hivyo akizidi umri huo anakuwa ni mtu mzima, sheria ya ndoa hususani vifungu vya 13-17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambavyo vimeweka bayana kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi au umri wa mahakama.

NINI JUKUMU LA SERIKALI ZA MITAA?

Michael Chigataa ni Afisa Mtendaji wa kata ya Ngwenda iliyopo Wilayani Chamwino mkoani hapa, anasema ndoa za utotoni katika kata yake zipo lakini si nyingi kutokana na jamii kutokuwa na elimu/uelewa wa kutoa taarifa katika ofisi za serikali za mtaa wakihisi kuwa si sahihi .

“Kesi za mimba na ndoa za utotoni zipo hapa kwenye kata yetu, ila jamii bado haitoi taarifa ya watuhumiwa lakini sisi tunachofanya tukisikia tetesi tunaenda kufuatilia mpaka tunampata mtuhumiwa  na kumfikisha sehemu husika na sisi tunaendelea kutoa wito kwa  jamii isivifumbie macho vitendo hivi pale vinapotokea  watoe taarifa ili  wahusika wachukuliwe hatua,”anasema Chigataa.

Naye Samweli Lungwa Mwenyekiti wa mtaa wa Mazengo uliopo katika kijiji cha Nkulabi Wilaya ya Dodoma mjini anasema elimu inaendelea kutolewa kwa jamii kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni sambamba na kuwataka wananchi watoe ushirikiano pale yanapotokea matukio haya.

“Jamii tunayoishi imezoea masuala ya kumalizana wao kwa wao mfano familia ya mzee fulani kijana amempa mimba mtoto, wazazi wanaenda kukaa na kuyamaliza wenyewe bila kushirikisha viongozi wa mtaa hii hali inatuharibia watoto na inazima ndoto za watoto walio wengi”anasema Lungwa.

DAWATI LA JINSIA.

Christa Kayombo ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Dodoma anasema Dawati linaendelea kukabiliana na kutokomeza ndoa za utotoni kwa kutoa elimu katika shule ya msingi, sekondari, vyuo pamoja na watoto waliopo chini ya miaka 18.

“Tunatoa elimu kwa mtu yoyote ambae yupo chini ya miaka 18  tunaelimisha jamii kwamba mtu mwenye umri wa miaka 18 ukifanya naye mapenzi unakuwa umembaka na kama mtu yoyote atapewa mimba akiwa chini ya miaka 18 tunafungua kosa la kubaka, kwa sababu ndoa  hiyo itakuwa imetokea kutokana na kitendo cha kubakwa, japo kuna wengine wanadhani wakikubaliana anakuwa hajabakwa lakini sisi tunasema akikubali ni amekubali kwa sababu ya utoto wake mtu mzima umemrubuni  kwa kutumia udhaifu wake wa utoto”amesema  Kayombo

Kayombo anasema ndoa za utotoni na vitendo vya ubakaji vinaripotiwa kwenye madawati na  ni dhahiri kwamba tatizo hilo lipo katika jamii  na idadi ya wanafunzi  wanaopata mimba za utotoni wapo anasema Jeshi la Polisi mchango wake umekuwa ni mkubwa katika kufatilia kesi mara tu tatizo hilo linapogundulika.

“Ili kukomesha vitendo hivi sisi kama dawati la Jinsia Mkoa tunapeleleza kesi hizi kuanzia tukio lilipotendeka hadi hatua za mahakamani, tunafanya kazi kwa weledi na ufanisi na kuharakisha upepelezi tunafungua hizi kesi katika madawati yetu kwa usiri ili tuweze kupata taarifa muhimu ili ziweze kutusaidia” anasema Kayombo

Aidha Kayombo anatoa wito kwa jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi   pale yanapotokea matukio ya ndoa hizo kwa kutoa taarifa na kusema kuwa jamii iache mazoea ya kumaliza kesi wenyewe.

“Sisi tunafanya kazi tunataka jamii ione kuwa mtuhumiwa aliyefanya kosa anafungwa miaka 30 au kifungo cha maisha mara baada ya kukutwa na hatia, tunaomba jamii itupe ushirikiano, Jeshi la polisi haliwezi kutabili na jamii tunaiomba iache tabia ya kumalizana wenyewe kwa wenyewe kwani kwa kufanya hivyo tunafuga waharifu na wataendelea kuwa kwenye jamii”anasema Kayombo

 


Post a Comment

0 Comments