IPO HAJA YA KUENDELEA KUDHIBITI MABADILIKO YA TABIA NCHI

 

Shamba la Mahindi likiwa limekauka kutokana na ukame.Picha kwa hisani ya Mtandao.

📌RHODA SIMBA

KUTOKANA na Mabadiliko ya  tabia nchi kuendelea kuleta athari kama ukame na joto kali kote ulimwenguni,hivi karibuni mjadala muhimu ulitawala katika mkutano wa COP 27 huko nchini Misri kuona ni kwa kiasi gani joto litapunguwa.

Pamoja na mataifa mengine ambao ni washirika muhimu katika mkutano huo kujadili njia ya kunusuru hali,lakini mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania,inaona wakati wa mataifa makubwa ulimwenguni wanatimiza ahadi ya kutoa fedha ili kunusuru mazingira.kutokana na ukweli kwamba mataifa yaliyoendelea yanayochangia mabadiliko ya hali ya hewa kutoka na shughuli za viwanda.

Angalau asilimia 99, ya wanasayansi wanakubali kwamba mabadiliko ya hali ya hewa ni ya kweli na yamesababishwa na shughuli za kibinaadamu na kubainisha kwamba Tangu 1850, wastani wa joto duniani umeongezeka kwa 1.1C.

Tunaona kwamba mabadiliko ya tabia nchi kwa sasa yamesababisha madhara mbalimbali ikiwamo njaa kwa jamii ambayo ilizoea kuzalisha chakula kwa wingi na kunufaika. Hali kadhalika kwa wafugaji kukosa sehemu za malisho ya mifugo yao tofauti kabisa na hali ilivyokuwa zamani.  Kufuatia hali hiyo, mabadiliko haya yameharibu na kuua  baadhi ya maeneo yanayojihusisha na  shughuli za kilimo na ufugaji ikiwemo  mkoa wa Dodoma.

John Nungu ni mkulima wa  zao la mpunga pamoja na mahindi na mfugaji  kutoka kijiji cha Ngulugano kilichopo wilayani Bahi mkoani Dodoma. Anasema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zake za kilimo na mazao hivyo kutovuna kama alivyozoea huku mifugo yake ikikosa sehemu za malisho Nungu anasema alitegemea kilimo na ufugaji  kwa ajili ya kuendesha maisha yake ya kila siku.

“Mabadiliko ya tabia nchi kwa sasa  yametuathiri sana sisi wakulima na wafugaji. Zamani tulizoea mvua zikianza kunyesha  mwezi wa 10 na 11. Wakulima tunakuwa tunalima lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kwa sasa tunafika hadi mwezi wa kwanza mvua hakuna, aidha  inachelewa kuja na kuwahi kuondoka hivyo kuacha mazao yakiwa  yamedumaa,” anasema na kuongeza.

“Kwa sasa nashauri elimu itolewe ili tusilime kwa mazoea. Tuanze kulima kilimo kinachoendana na  mvua ambayo inaendana na hali ya hewa kwa sababu mpaka sasa tunaamini ya kuwa wananchi hatuna uelewa kuhusu masuala haya ya mabadiliko ya tabia nchi. Wengine wanafika mbali zaidi na kuamini kuwa  mvua zinasababishwa na utawala wa kiongozi fulani kwa wakati huo. 

 Na wengine wanasema  kuwa kuna ushirikina ambao unazuia mvua, mfano zamani  mimi  nilikuwa nikilima heka moja  napata gunia  20 za mpunga, lakini kutokana na hali ya sasa hivi, heka moja  unaweza ukatoa gunia kumi, na kuna wakati tunakosa  kabisa unaweza pata gunia tano

 anasema bwana Nungu.

Hali hii imesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamesababisha ukame katika baadhi ya maeneo ikiwemo Dodoma na hii imesababisha kuwepo kwa mfumuko wa bei ya vyakula ambavyo kwa sasa vinauzwa kwa gharama ambayo wananchi wanashindwa kuimudu.

kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa ya Dunia-WMO  joto limeendelea kuongezeka duniani pamoja na kina cha bahari.

Mabadiliko ya tabia nchi ni matokeo ya kuongezeka kwa joto duniani kwa sababu ya kuharibika kwa tabaka la Ozoni yani Ozone layer, tabaka hilo hupunguza mionzi ya jua inayokuja duniani, lakini linaharibiwa na uharibifu wa mazingira hasa shughuli za binadamu.

Janeth Lwabe  ambae pia ni mkulima wa mazao mchanganyiko ikiwemo  karanga, mtama na  mahindi kutoka kijiji cha Nkulabi kilichopo jijini Dodoma, anasema kilio chake ni  kwa  serikali  pamoja na wadau wa mazingira nchini kuona ni kwa namna gani wanaweza shirikiana katika kuhakikisha wanarudisha hali ya hewa ya  mvua na mazao yashamiri kama ilivyokuwa zamani.

“Zamani tulikuwa hatutumii nguvu nyingi ukilima unajihesabia kabisa wewe umepona na njaa, lakini siku  hizi tunaogopa hata kuwekeza nguvu nyingi katika kilimo maana unaweka mazao mengi lakini wakati wa kuvuna unaweza jikuta unavuna isifike hata kile kiasi cha mbegu ulichopanda na zamani hata mbolea ilikuwa ni rahisi kuipata kwasababu mifugo ilikuwa inapata malisho ya kutosha yanayozalisha mbolea.

“Wadau wa mazingira  tuwaombe watoe elimu kwa jamii ya namna ya utunzaji wa mazingira mfano huku kwetu suala la ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa  limeshamiri   kiasi kwamba mashambani siku hizi hakuna hata miti, wakati zamani  mashamba yalikuwa  yamejaa miti ya kivuli kibao ukichoka kulima unapumzika,”anaesema Bi Janeth.

Athari za mabadiliko ya tabia nchi zimejidhihirisha kwa zaidi ya miaka 50 sasa ambapo hali ya hewa duniani imekuwa ikibadilika, kwa sababu ya kuongezeka gesi chafu zinazozalishwa na mvuke wa maji na hewa ya ukaa.

Gesi hizo zinatokana na kuungua kwa mafuta na makaa ya mawe, ukataji wa miti na shughuli nyingine za kibinadamu kama kilimo na uchimbaji wa madini na shughuli za viwandani.

Kauli ya Serikali

Samweli Lungwa ni mwenyekiti wa kijiji cha Nkulabi kilichopo jijini Dodoma. Anasema mchango wao katika kuhakikisha wananchi wanatunza mazingira ili  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na kuzuia suala la ukataji na uchomaji wa miti, na  mashamba ovyo bila utaratibu maalum.

“Sisi tunaendelea kuhamasisha wananchi wapande  miti kwa wingi kwa sababu zamani tulikuwa na mapori yenye  miti na ukisema unaenda porini ni pori kweli.  Kwa hiyo tunahamasisha  upandaji miti katika kila nyumba na ninawachukulia hatua watu wanaochoma miti ovyo na nimewaambia kabisa wananchi unapokata mti panda mti,” anasema Lungwa.

Senyagwa Nhonya  ambae ni Afisa Mtendaji kata ya Nghulugano iliyopo wilayani Bahi Mkoani Dodoma anasema wananchi katika suala la ukataji miti bado ni tatizo halafu wao ndio wanakuwa waathirika wa kwanza katika kuhangaika na  kusema  hawanufaiki  na  kilimo na malisho.

“Nikiwa kama Afisa Mtendaji  kwanza suala la kusafirisha magunia ya mkaa hapa  mpaka wawe na kibali maalumu lakini elimu ya upandaji na utunzaji wa mazingira bado tunaendelea kuitoa  hapa  kijijini chetu.  Lengo ni kuhakikisha tunarudisha uoto wa asili kama zamani ilivyokuwa,

Nitoe wito kwa jamii suala la utunzaji wa mazingira si jukumu la serikali bali ni letu sote tuhakikishe basi unapokata mti panda mti mwingine ili kufidia ule ulioukata

 Senyagwa Nhonya

 

MCHANGO WA MABALOZI WA MAZINGIRA NCHINI

Sakina Abdulmasoud ni balozi wa mazingira nchini Tanzania anasema kazi yao mabalozi wa mazingira ni kuitafsiri kwa vitendo ajenda ya mazingira kwa kuhamasisha jamii ione umuhimu wake na kulifanya suala la upandaji wa miti kuwa ni utaratibu wao kawaida.

"Kama unavyofahamu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inahamasisha upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kupitia  kampeni mbalimbali, ambapo sisi mabalozi jukumu letu kubwa ni kubeba ajenda ile na kuisogeza kwa wananchi kwa ajili ya utekelezaji,"

“Kazi zetu tunazifanya moja kwa moja kwa jamii, kupitia utoaji wa elimu mashuleni, uhamasishaji wa wananchi kwa kujumuika nao kwenye shughuli za upandaji wa miti, lakini miongoni mwetu wapo waandishi wa habari ambapo kupitia kalamu zao wanaelimisha jamii kwa kuwa tunafahamu ili kuiokoa nchi yetu katika hatari ya mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha  ukame katika baadhi ya maeneo  mafuriko na majanga mengine ni lazima tufanye kazi kwa ushirikiano,” anasema balozi Sakina.

Oliver Nyeriga nae pia ni  balozi wa mazingira anasema pamoja na jitihada zao za kupambana kwa vitendo kuhamasiha suala la utunzaji wa mazingira lakini  bado wana kazi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii kwani  kuna  baadhi yao ambao hawaoni haja ya utunzaji wa mazingira.

“Mfano sisi tunakwenda kwenye mitaa, masoko na  sehemu nyingine zenye mikusanyiko ili kuhamasisha suala la utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi lakini tunachotaka sisi jamii ione kama suala la utunzaji wa mazingira si lazima wahamasishwe na mtu wafanye kama wajibu wao kama yalivyo majukumu mengine wanayoyafanya ya kila siku bila kuhimizwa siku zote tunasema tunza mazingira yakutunze na usafi ni utu,” anasema  balozi Oliver

WADAU WENGINE WA MAZINGIRA

Njamasi Chiwanga  ni mkurugenzi wa miradi kutoka Shirika la LEAD FOUNDATION lililopo wilayani Mpwapwa, Dodoma,  linalojishughulisha na  utunzaji wa mazingira  kwa  uoto wa asili  anasema wao wana  mchango  mkubwa  na kwa sasa wana mradi wa KISIKI HAI shuleni ambao  upo katika shule 35 katika Mkoa wa Dodoma, Singida na Arusha unaosambaza  elimu ya mazingira katika jamii.

“Sisi Lead Foundation  licha ya kuwa tunafanya suala hili katika mazingira ya kawaida lakini pia tumeamua kuanzisha kampeni hii shuleni  ili kuweza kuwafikia watoto, kuwabadilisha  fikra zao wakiwa wadogo hata  wanapokuwa watakuwa mabalozi wazuri wa mazingira  na waswahili siku zote husema samaki mkunje angali mbichi.’’

“Mradi huu tayari umeshatolewa muongozo  wake  shuleni  tunasema lazima uanze kutunza mazingira ndipo uwaze kufikiria maendeleo ya kila mtu mmoja mmoja.  Tunapokaa tukizungumzia   biashara unagusa  mazingira, afya, maji, elimu. Vyote  hivi vinagusa mazingira na sisi kama Shirika tumemua kugusa agenda  za serikali katika utunzaji wa mazingira,” anasema Chiwanga.

Chiwanga anasema wao wanachofanya  hawapandi miti ila wanarudisha miti iliyokatwa kwa maana kisiki ambacho kipo hai ardhini lakini kilishakatwa juu wanakirudisha kinasimama tena na kuwa mti mkubwa ambao unaishi.

MAJUKUMU YA WASIMAMIZI  WA MISITU

Deosdedith Bwoyo ni  Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki kutoka Wizara ya  Maliasili na Utalii anasema  majukumu yao hasa ni kusimamia rasilimali  za misitu, afya ya misitu, pamoja na kulinda hifadhi ya misitu  isiharibiwe.

Anasema katika suala  la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi wao  kama wasimamizi  wakuu wa misitu katika ngazi zote,  wanapambana na uharibifu ambao unafanywa na shughuli za  kibinadamu  ikiwemo kukata miti au kufyeka  kwa ajili ya kupata mashamba, kuni, mkaa, mbao na kadhalika.

“Mfano mtu anakuta kuna shamba la miti  ambalo limestawi na lina afya sasa kutokana na haja yake yeye kwa wakati huo ya kutafuta mathalani kuni au mbao anaingia anakata, na wengine wanafika mbali zaidi akikuta kuna eneo ambalo limestawi vizuri kwa kuwa tu anaona kwamba akifyeka pale kwa kuwa pamestawi anahisi akipatumia kwa kilimo patastawi na kupata mazao mengi zaidi anaingia anakata na kuchoma.

Madhara haya ya  moto ambayo yamekuwa yakitokea katika baadhi ya misitu hapa nchini yanafanywa na wananchi ambao wamekuwa wakikata miti kwaajili ya matumizi yao na niseme mimi kama Mkurugenzi wa misitu   licha ya kuendelea kuwachukulia hatua wale ambao wamekuwa wakifanya uharibifu huo lakini elimu tunaendelea kuitoa juu ya utunzaji wa misitu hii.

Deosdetith Bwoyo

Akizungumzia kuhusu  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) Bwoyo amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa Wakala huo pia ni kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti, wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki unakuwepo na  kuongeza thamani ya mazao ya misitu na nyuki na kutoa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. 

Bwoyo amesema  dhima yao kuu ni usimamizi endelevu wa rasilimali za taifa za misitu na nyuki ili kuchangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Nitoe rai kwa wananchi kuacha tabia ya kuchoma misitu ovyo siku zote tunapotunza hii misitu inakuja kututunza sisi mfano tukitembelea ndani kwa kila mtu hapa nchini kwetu, unakuta ana meza ana kitanda ana kabati hivi vyote vinatokana na miti hii ambayo ipo kwenye misitu sasa ikikatwa zaidi itafika mahala tutakosa haya mahitaji,” anasema Bwoyo.

 

Post a Comment

0 Comments