TMA: TUMEBORESHA MIUNDOMBINU HUSUSANI UJENZI VITUO SABA VYA RADA VITAKAVYOANGAZA NCHI KWA SAA 24.

📌RHODA SIMBA

MAMLAKA ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 imeboresha sekta  ya mamlaka hiyo kwa kuanzisha  miradi mbalimbali, miundo mbinu hususani ujenzi wa  vituo vya rada saba  pamoja na vifaa ambavyo vitasaidia kuangaza nchi masaa 24.

Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini Dodoma Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri - Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa amesema kuwa licha ya kuanzisha miradi hiyo tayari wataalamu wamepatiwa mafunzo  kwa ajili ya kuendesha rada hizo.

Mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani aidha, utengenezaji wa rada mbili za mwisho zitakazofungwa KIA na Dodoma umefikia asilimia 45 ambapo Mamlaka ilifungua barua ya dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya utengenezaji wa Rada hizo

Kukamilika kwa rada hizi kutakamilisha mtandao wa rada nchini kwa idadi ya rada saba, rada hizi zina uwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250

Dkt. Kabelwa.

Akizungumzia mikakati ya mamlaka hiyo Dkt Kabelwa amesema mamalaka hiyo imejipanga kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa na kuendelea na utekelezaji wa Sheria Na.2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake.

Tumedhamiria kuimarisha uangalizi wa hali ya hewa katika bahari na maziwa makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia

Tumejipanga kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini na kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake

Dkt Kabelwa

Aidha mpango mwingine amesema ni kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa, kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

Amongeza kuwa Mamlaka imeendelea na juhudi za kuongeza mapato kwa kuwafikia wadau mbalimbali na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa ambapo amesema jitihada  zimepelekea mapato ya Mamlaka kuongezeka kwa asilimia 53% katika mwaka wa fedha 2021/22. 

Mamlaka imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza gharama za uendeshaji wa Taasisi ambapo imeweka mkazo katika kutumia TEHAMA kwa ajili ya uendeshaji na utoaji wa huduma. Mifumo hiyo pia imeiwezesha kutoa huduma mahsusi kwa sekta za madini, usafiri wa barabara, ujenzi na utalii

Hata  hivyo  Dkt Kabelwa amesema Mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya tafsiri ya taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali ambazo hazina usahihi juu ya masuala ya hali hewa na vipindi vya mvua hapa nchini.

 

 




Post a Comment

0 Comments