VITA YA UKATILI WA KIJINSIA BADO SAFARI NDEFU.

 

📌RHODA SIMBA

Maeneo mbalimbali  duniani yamekuwa yakikabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, changamoto hiyo, licha ya jitihada zinazofanywa, lakini bado inaonekana kushika kasi. 

Mathalan, nchini Tanzania, ripoti bado zinaonesha kwamba asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika maishani yao. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na  Wizara ya Maendeleo ya Jamii  Jinsia, Wanawake  na Makundi Maalum mwaka 2021.

Miongoni mwa wanawake walliokabiliwa na masaibu hayo nchini Tanzania ni pamoja na Zilipa Zebadayo, 39, mkazi wa kijiji cha Nagulo kilichopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Akimwelezea mwandishi wa makala hii, Zilipa anasema yeye amewahi kuolewa akiwa na umri wa miaka 19 na mwanamume aliyemzidi umri.

Anasema chanzo cha kuolewa kwake ni kutokana na hali ngumu ya maisha na kukosa kitu cha kujishughulisha.  Na hili limetokea pindi tu alipomaliza darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo. Kama ilivyo kwa idadi kubwa ya wasichana wanaomaliza kusoma na kushindwa kuendelea, nae alienda   jijini Dar es Salaam kama mfanyakazi wa ndani. 

Nilichoka kufanya kazi za ndani nikaonanirudi nyumbani ili nipate mchumba niolewe. Nikapata mchumba wa hapa hapa kijijini kwetu, tukafunga  ndoa  mwaka 1999.  Baada ya wiki tu, vipigo vikaanza. Nilikuwa napigwa mpaka nazimia.  Halafu majirani zangu wote walikuwa wanaogopa kuja kuamua ugomvi wetu nikianza kupigwa

Zilipa 

Taarifa hiyo imeongeza kusema kuwa asilimia 20 ya wanawake wamefanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 9 ya umri kati ya miaka 15 hadi 49 wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.  

Wakati huo huo, imearifiwa kwamba, katika jamii baadhi ya malalamiko hayo ya ukatili wa kijinsia hayaripotiwi na baadhi mengine kutosikilizwa au kufanyiwa kazi pindi yanapotolewa.

Zilipa anasema hali hiyo ya manyanyaso na kipigo iliendelea mpaka akaja akapata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza  anasema aliwahi kupigwa mpaka  mimba ikataka kuharibika. 

Mimba iitaka  kuharibika ya mwanangu wa kwanza yani kuna wakati unapigwa tuu unakuta ana visababu vingi mfano mbona mboga ina mafuta  ugali haujaiva, kwa kweli nimepitia kipindi kigumu mno nikaja nikajifungua mtoto wa kwanza sijapumzika nikapata ujauzito wa pili hali ikaendelea  akaja akanipiga mpaka akaning’oa meno yangu mawili ya mbele nikaenda kuripoti ofisi ya serikali za mtaa wakasuluhisha ile kesi tukafika mahakani tukaja kukubaliana tuachane ila atimize wajibu wake wa kutoa huduma kwa watoto, basi mpaka sasa ameendelea na maisha yake nami pia  sema ndio hivyo kaniachia kilema cha kutokuwa na meno ya mbele

 Zilipa.

Lakini sio wote wenye ujasiri wa kutoa taarifa kama aliokuwa nao Zilipe.  Elice Chigataa, 50, ambaye ni mama wa watoto watano nae yalimpata kama ya Zilipa.

Mama huyu ambae ni mkazi wa kijiji cha Nghambi  kilichopo Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, anasema yeye aliwahi kuolewa na kuishi na mumewe kwa muda wote mpaka anafariki, lakini  alikuwa akipitia ukatili wa kupigwa hadi kuchomwa na moto na hakuwa na uelewa wapi anaweza akaenda kusema.

Nilikuwa napigwa. Anachukua moto wa kuni ananichoma mikononi, lakini kila nikikimbia kwetu. akija anasema atabadilika, narudi kuishi nae, lakini habadiliki. Mkikaa siku mbili akilewa tu anaanza tena ukorofi na ananambia utaenda wapi ukisema polisi nitakupiga nikuuwe kwa hiyo nikawa sielewi wapi  pakusemea matatizo yangu. Nimeteseka  kwa kipindi hiki chote mpaka kifo kilipokuja kumchukua,

 Elice. 

Baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wanakiri kwamba, uhaba wa elimu miongoni mwa waathirika kutojua wapi watoe taarifa ni moja wapo ya changamoto, lakini pia kukosa ujasiri. 

Hata hivyo, suala la ukatili halipo kwa wanawake pekee, ripoti mbalimbali zinaonyesha wanaume pia ni waathirika. Ingawa wanaume wanaona aibu kuripoti wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. Hii pia inatokana na fikra hasi za watu kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa sababu jamii nyingi hazizungumzi kuhusu ukatili kutokana na uwepo wa mila na desturi na mifumo dume.

Ndewa Elia ni mwanamke mwenye umri wa miaka 37  mwenye watoto watano  mkazi wa kijiji cha Nkulabi kilichopo jijini Dodoma anasema chanzo cha yeye kufanyiwa ukatili na mume wake, ni baada ya mumewe kukaidi ushauri wa wataalamu wa afya wa kumtaka yeye ajifungue katika hospitali ya rufaa. 

Alikataa niende kujifungua mjini kwa madai kwamba gharama za mjini ni kubwa. Baada ya kumlazimisha akanambia sikuzikikaribia nitaendea, basi nikasubiri siku zimeenda kila nikimkumbusha anakuwa mkali, mpaka siku nimeumwa uchungu usiku akaniacha akanifungia ndani akaondoka.

Usiku ule nilipata uchungu wa uzazi mpaka nikajifungulia ndanii peke yangu. Nilipiga kelele majirani zangu wakaja kunisaidia  usiku ule huku wakiniuliza  mumeo yukwapi nikawaelezea hali halisi

Ndewa

Baada ya kupata msaada huo, Ndewa alishauriwa na majirani kwenda kutoa taarifa polisi, lakini kwa masikitiko, anasema, alihuzunishwa na majibu aliyoyapata polisi. 

Niliambiwa nitoe hela ili kesi iweze kuendelea. Niliposema sina hela kwa sababu nimetoka kujifungua, nikaambiwa nikapumzike

Baada ya kuwa mwanangu amekuwa kidogo nikarudi tena kituoni kuulizia wakaniambia wao hawasuuhishi wala kuachanisha  mke na mume turudi tukazungmze na  kuyamaliza  nyumbani 

Ndewa.

Kauli ya polisi kuhusiana na tuhuma za rushwa  pale jamii inapoenda kuripoti tukio la ukatili inasema huduma hiyo inatolewa bure bila malipo  na endapo mwananchi akafika kituo cha polisi na akakutana na askari anaekiuka maadili akataka  rushwa  apige simu  bure ya polisi ya 113.  


Wanaharakati wa kupinga ukatili wa jinsia wanazungumza

Zakia Msangi ni mwanasheria kutoka Shirika la Wanawake linalotumia sheria kumuokoa mwanamke na mtoto anayepitia ukatili wa kijinsia WILDAF. 

Shirika lao muda mwingi limekuwa likipambana na masuala ya kupinga kwa kiasi kikubwa  ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni kwa kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya matamasha.

Zakia anasema  mfumo wa kuripoti taarifa za ukatili  wa kijinsia  ni rafiki kwa jamii kwakuwa sasa kuna madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi wanaosikiliza na kuhudumia  kesi hizo.

Mfumo ni rafiki sema tunachoendelea kusisitiza jamii  ione suala hili la kuripoti ni suala  la kawaida  si kitendo cha aibu na kwa sasa kuna  Ofisi za Ustawi wa Jamii zilizoko kila kata hasa kwenye kesi hizi za ukatili wafike kutoa taarifa zao

Zakia.

Akizungumzia kuhusu mchango wa WILDAF anasema wao  wanatoa msaada wa kisheria kwa wahanga  ambao tayari wamefanyiwa vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia bure bila malipo yoyote.

Naomi Gerald  ni Afisa Miradi Kutoka Shirika la Rafiki  lililopo Mkoani Shinyanga anasema ili kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia  wao wanatoa elimu za jinsia kwa vikundi ambavyo wamewawezesha  mabinti kwa ajili ya kujikwamua Kiuchumi.

Tunawatengenezea vikundi hivi  ili kuepukana  na vitu ambavyo vitawapeleka kwenye ukatili wa jinsia  unajua kitendo cha kukosa kitu cha kujishughulisha nacho  Moja  kwa Moja hata akienda kuolewa atanyanyasika.

Sisi kama Rafiki tumewatengenezea mabinti biashara ya  kukopeshana wanatengeneza sabuni,karanga mikoba Ili wajipatie vipato na kupitia miradi ambayo tunaifanya hizo kesi zipo  na tulitambua kuwa hilo tatizo lipo na  ndio maana tunaenda kupambana nalo kwa kuwapa mtaji mabinti wafanye ujasiriamali

Jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa mashirika haya ambayo yanafanya harakati za kupinga  ukatili  iwe tayari kufikiwa na  kupata elimu kwaajili ya kujikinga na  kupata elimu juu ya ukatili

Kwa kiwango  kikubwa sisi tunakutana na wazazi kupitia  vijiwe mbalimbali ikiwemo vijiwe vya kahawa tunawapatia Elimu kuhusu kupinga  ukatili pamoja ndoa za utotoni pia tunawaelimisha mabinti. 


Nini kauli ya dawati la jinsia?

Christer Kayombo ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Dodoma anasema kasi ya kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia kwa sasa imekuwa kubwa tofauti na hapo zamani ambapo watu walikuwa wakinyamaza pale wanapofanyiwa ukatili.

Sisi kama dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma vitendo hivi  vya ukatili vinaripotiwa na  ili kukabiliana na tatizo hili la ukatili   kwanza kabisa tunaendelea kutoa elimu ya aina ya makosa ambayo mtu ama jamii ikifanyiwa ione kabisa kuwa ni ukatili wa kijinsia

Tunatoa elimu kwenye jamii, shule za sekondari, msingi, vyuo mbalimbali. Tunatoa elimu kwenye vyuo kwa sababu huko bado kuna watoto na ili kukomesha vitendo hivi sisi kama dawati la jinsia mkoa tunapeleleza kesi hizi kuanzia tukio lilipotendeka hadi hatua za mahakamani.  Tunafanya kazi kwa weledi na ufanisi kuharakisha upepelezi. Tunafungua hizi kesi katika madawati yetu kwa usiri Ili tuweze kupata taarifa muhimu ili ziweze kutusaidia

Kayombo.

Kayombo anasema jamii inaishi na waharifu  ambao tayari walishawafanyia watu ukatili  lakini hawajafikishwa popote, na anaongezea kuwa wao kama dawati la jinsia wanataka  kazi wanayoifanya  jamii ione kuwa mtuhumiwa kafungwa miaka 30 au kifungo cha maisha.

Wito  wangu kwa jamii itoe ushirikiano, wanapoona viashiria hivi vya ukatili wa kijinsia waripoti kwani jeshi la polisi haliwezi kutabiri na waache ile tabia ya kumaliza kesi zao majumbani. Hii inawaumiza waathirika waliofanyiwa vitendo vya ukatili

Kayombo 

 

Post a Comment

0 Comments