BAHI YAONGOZA KUKAMILISHA UJENZI WA MADARASA

📌MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amekabidhiwa vyumba 14 vya madarasa na ofisi 9 za walimu zilizokamilika kwa fedha zilizotolewa na Serikali kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 waweze kupata madarasa ya kutosha ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.

Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ikiwa ni miongoni mwa Halmashauri 8 za mkoa wa Dodoma zilizopewa fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa ilipokea shilingi Milioni 280 tarehe 8 Oktoba, 2022 na imeweza kuwa Halmashauri ya kwanza kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo na kukabidhi tarehe 12 Disemba, 2022 huku kila darasa likiwa na viti 40.

Akisoma taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Bwana Athumani Masasi amesema kuwa

Vyumba vya madarasa 14 na ofisi 9 vimejengwa katika shule zote 8 za Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ikiwemo shule ya sekondari ya Bahi iliyokabidhi vyumba 5 na ofisi 2, Idihwa darasa 1 na ofisi 1, Kigwema madarasa 2 na ofisi 1, Chikola darasa1 na ofisi 1, Chipanga darasa 1 na ofisi 1, Chibelela darasa 1 na ofisi 1, Msisi Juuma madarasa 2 na ofisi 1 na Lamaiti darasa1 na ofisi 1.

Aidha Mhe. Senyamule ametoa pongezi kwa Halmashauri hiyo na kutaka iwe ya mfano kwa Halmashauri nyingine zilizopo ndani ya Mkoa na kusema;

Mhe Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ana nia ya dhati ya kutaka kuondoa ujinga kwa kuimarisha sekta ya Elimu ambapo ametoa fedha za kuongeza vyumba vya madarasa 8,000 nchi nzim ambapo kwa Mkoa wa Dodoma tumepata jumla ya vyumba vya madarasa 339

Senyamule

Sambamba na hilo Mhe. Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwa kuweza kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2022 kwa kuweza kuwa katika orodha ya Shule 10 bora zilizofanya vizuri kitaifa ambapo kwa Mkoa wa Dodoma ni Halmashauri hiyo pekee ndiyo iliyoweza kuingia katika 10 bora.

Hata hivyo RC Senyamule ameongeza kuwa Mhe. Rais ametekeleza miradi ya maendeleo kwa zaidi ya asilimia 80 kwa Mkoa wa Dodoma huku vituo vya afya, zahanati, madarasa na huduma zingine zikizidi kuimarishwa.


 

Post a Comment

0 Comments