SERIKALI KUWEKA MIFUMO MADHUBUTI YA KUWANASA WOTE WANAOTOA NA KUPOKEA RUSHWA.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro kuelekea siku ya maadili na haki za binadamu amezungumza namna serikali ilivyojipanga kukabiliana na vitendo vya rushwa hasa katika Ofisi za umma ambapo amesema tayari wameweka mifumo madhubuti ya kuwanasa wote wanaopokea na kutoa rushwa katika kuhudumia wananchi.

Dkt.Ndumbaro ameyaeleza hayo Jijini Dodoma katika hafla hiyo ambapo amesema kuwa juhudi za kupambana na rushwa zinaifanya Tanzania kuendelea kuaminiwa hivyo, wawekezaji kuendelea kuja kuwekeza nchini, kuendelea kupata mikopo na misaada mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa vituo vya Afya, shule na miundombinu mingine muhimu ikiwemo ya usafirishaji.

Rushwa ni tatizo katika nchi nyingi duniani hivyo mwaka 2003, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilikubaliana kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa kila tarehe 9 Desemba kuanzia mwaka 2004 ikiwa ni fursa mojawapo kwa kila nchi kutathmini juhudi zake za kudhibiti vitendo vya rushwa

Wote ni mashahidi kuwa uwepo wa vitendo vya rushwa unaifanya Serikali kushindwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuwahudumia wananchi ipasavyo, Hii ni kwa sababu miradi ya maendeleo hufanyika kwa kiwango cha chini kutokana na fedha zinazotengwa kutekeleza miradi hiyo, kuingia katika mikono ya watu wachache,"amesema.

Aidha amesema kuwa serikali imeendelea kutoa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu nchini, kadhalika, huduma za afya nchini zimeimarika kutokana na juhudi kubwa ya Serikali ya awamu ya sita kusimamia kwa karibu ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na majengo katika Hospitali za Wilaya, na  Mikoa. 

Pia Serikali imeendelea kutoa elimu bure kuanzia shule za Msingi mpaka sekondari kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye uwezo wa kusoma anapata haki hiyo aidha, katika ngazi ya vyuo vya kati na vya elimu ya juu, serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kupata haki ya elimu katika ngazi hiyo ambapo kwa ujumla, miradi mingi inayoendelea nchini, inalenga kuboresha maisha ya mtanzania.

Ikumbukwe kuwa tafiti iliyofanywa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Tanzania TAKUKURU ilibainisha Taasisi zinazoongoza kwa rushwa ni Polisi, Sekta ya Afya, Mahakama na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA‎.

Ikiwa takwimu za Amnesty International zinaonyesha hali ya rushwa nchini Tanzania kwa mwaka 2021 ilipata alama 39 na kupanda kutoka nafasi ya 97 mwaka 2020 hadi nafasi ya 94 kati ya nchi 180 hali ambayo baadhi ya wananchi wamesema bado vitendo vya rushwa kiuhalisia vinafanyika na kuwanyima kupata huduma na haki zao za msingi kwa baadhi ya maofisi.

Kwa upande wake afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka ya kudhibiti ununuzi wa umma PPRA Eliakim Maswi alisema kuwa PPRA ni sehemu katika Taasisi zinazosimamia maadili katika utumishi wa umma na wao wanasimamia ununuzi wa umma kwani kama hakuna maadili hawategemei kupata thamani ya Fedha halisi ya ununuzi na pia kuona ufanisi katika utekelezaji wa ununuzi wa umma.

Sisi tunaamini kwamba kukiwa na maadili ya ununuzi wa umma basi tutaleta ufanisi na huduma inayotolewa kwa wananchi wa Tanzania itakuwa inawafikia ipasavyo

Pia alieleza kuwa mpaka sasa zipo taasisi 837 zinazotumia mfumo na lengo ni kuhakikisha wanathibiti na kuendeleza maadili katika Serikali na ndipo Serikali ilianzisha mfumo mpya utakaoanza kutumika mwaka mpya wa fedha na mfumo huo utaongeza ufanisi zaidi na utaongeza uwazi zaidi na kudhibiti matumizi ya Fedha za umma katika ununuzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma wamesema bado kuna baadhi ya watendaji katika Ofisi mbalimbali wana tamaa ya mali na kuvunja sheria kwa kudai rushwa kwa wateja ili wawasaidie huku wengine wakidai wananchi pia ndio wanashawishi kutoa rushwa ili wapate huduma kwa muda mfupi. 

Saleh Ramadhani ni mkazi wa Dodoma amesema kuwa akienda katika baadhi ya Ofisi bado kuna changamoto ya rushwa kwani watu ambao wanatanguliza rushwa bado wapo na kuiomba Serikali iendelee kutoa elimu na kuweka mkazo katika sheria zilizopo kwa yule atakaye pokea na kutoa rushwa.

Ipo haja ya serikali kuendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kata kwa wenyeviti wa mitaa na mabalozi inatakiwa waendelee kutoa elimu kwa wananchi juu ya vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na kuweka mkazo katika sheria zilizopo

Ramadhani.

Huku Felister Richard amesisitiza kuwa suala la elimu kuanzia ngazi za chini hasa shuleni awali ili mwananchi awe na mazoea ya kutokujihusisha na vitendo vya rushwa.

Elimu izingatiwe na isitolewe juu juu inatakiwa itolewe kuanzia ngazi ya chini kabisa kwa shule ya msingi itasaidia kukua ukiwa unajua kuwa vitendo hivyo sio vizuri kwa jamii na mfano unakuta mtu hana uelewa juu ya rushwa akifika Hospitali anaumwa uchungu muuguzi anataka rushwa anaona atoe ili aokoe maisha yake

Kama mnavyokumbuka mwaka 2016 Serikali ilianza kuadhimisha siku mbili za Kimataifa tarehe 10 Desemba ya kila mwaka: yaani Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambazo kwa Tanzania ni Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu,Hivyo, huu ni mwaka wa sita (6) kwa maadhimisho haya kufanyika kwa pamoja.



 

 

Post a Comment

0 Comments