TAKUKURU KUFANYA VIPIMO VYA RUSHWA KWA MIKOA.

 

📌RHODA SIMBA

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kufanya vipimo vya rushwa na kuitangaza ile Mikoa itakayoinekana ina kiwango kikubwa cha Rushwa ili iweze kujitafakari.

Kadhalika amemuagiza Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU kuhakikisha Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na wanapotekeleza majukumu yao wasimuonee mtu kwa kumbambikizia.

Waziri Mhagama ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa TAKUKURU pamoja na uzinduzi wa program ya TAKUKURU rafiki yenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wananchi kuanzia ngazi ya Kata ili kuongeza nguvu ya mapambano katika kuzuia rushwa isitokee katika Jamii.

Mapambano yenu mnayapeleka katika kupambana na Rushwa lakini haitukatazi na haituondoi kwenye majukumu yetu ya kila siku majukumu tuliyopewa ni ya kushughulika na kupambana na rushwa ujenzi wa maadili na stahiki kwa watumishi wa umma

Nyie makamanda wangu wa Mikoa mahali pa kuanza ni kwa huyo Katibu Tawala msaidizi anayeshughulikia Utawala na rasilimali watu akiweza huyo kufanya kazi zake vizuri mienendo na vitendo vya ubadhulifu wa fedha za taifa hili kwenye Halmashauri zitapungua ama kuisha kabisa kutaneni nao hawa

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishina wa Polisi CP Salum Hamduni amesema Tanzania ni moja ya nchi sita duniani zilizotangazwa  kupiga hatua katika masuala ya mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini.

Nchi nyingine zilizopiga hatua ni pamoja na Ethiopia, Sisheli, Angola, Rwanda na Senegal ambazo zimepiga hatua kutokana na utafiti uliofanywa na mashirika mbalimbali likiwemo la Transparent International.

Amesema mafanikio hayo ni makubwa sana kutokana na awali walikuwa nafasi za mbali katika mapambanaji dhidi ya Rushwa.

Mkurugenzi Hamduni amesema pia wamepanda nafasi ya 87 kwa mapambano dhidi ya Rushwa kati ya nchi 187 ambazo zimefanyiwa utafiti na mashirika mbalimbali.

Tunashukuru kufikia nafasi hiyo na imani tutaendelea kupanda zaidi nafasi za juu katika mapambano dhidi ya Rushwa,"alisema Mkurugenzi huyo.

Amefafanua zaidi ya kuwa mapambano dhidi ya Rushwa ni ya kila mmoja hivyo kila mtu anapaswa kumuangalia mwenzake anayehusika na vitendo dhidi ya Rushwa.

Akizungumzia kuhusiana na uzinduzi wa program Rafiki ya kupambana na Rushwa amesema itapelekwa kila mahali mpaka kwenye kata ambapo itawasaidia wananchi kujua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo hayo.

Amesema ni jukumu la kila mmoja kupambana na Rushwa na si Taasisi pekee hivyo wanapaswa kutoa taarifa ambazo zinaviashiria vya rushwa.

Amesema mkutano huo ni kwa ajili ya kuangalia na kutoa tathmini ya utendaji kazi zao za kila siku katika maeneo mbalimbali hapa nchini.


Naye Naibu Mkurugenzi wa Takukuru Neema Mwakalyelye alisema mkutano huo umehusisha makamanda kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Amesema uzinduzi wa program hiyo utasaidia jamii kujua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo wanayoishi hivyo kila mmoja ni wajibu wake kupambana na Rushwa.

Hata hivyo ameshukuru serikali kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha Rushwa inapigwa vita katika maeneo mbalimbali hapa nchini.



 

Post a Comment

0 Comments