TANZANIA KUUNGANA NA MATAIFA MENGINE KUADHIMISHA SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

TANZANIA imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu. Serikali imewataka viongozi wote wanaosimamia utoaji huduma katika sekta ya umma na binafsi kuwajibika na kusimamia utoaji wa huduma bila kudai au kupokea rushwa.

Akizungumza katika siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa yaliyofanyika Jijini Dodoma Prof. Ibrahim Khamiss Juma amewataka viongozi kutimiza ahadi ya uadilifu kwa umma.

Profesa Juma amesema kumekuwepo na vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa ahadi za uadilifu kwa upande wa viongozi na watumishi wa umma na sekta binafsi.

Amesema kuwa misingi ya Maadili ya Viongozi wa umma, ipo kwa mujibu wa Ibara ya 132 (5)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni pamoja na, kupiga marufuku mienendo na tabia zinazopelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii.

Tukumbuke kuwa, watumishi wa Umma wanaojihusisha na vitendo vya rushwa huwakosesha wananchi haki zao za msingi, ustawi wao, na wa Taifa.  Kwa kufanya hivyo watambue kuwa, wanafanya vitendo vya kijinai, na pia, wanakiuka Haki za Binadamu na kwamba wanavunja Ibara ya 12 - 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977

Prof.Juma

Aidha amesema kuwa mafanikio katika vita dhidi ya rushwa vinategemea pia wananchi kukataa kutoa rushwa pale wanapoombwa na hutegemea  kama watakuwa tayari na wepesi kutoa taarifa pale wanapoombwa rushwa na wajitokeze kutoa ushahidi Mahakamani.

Kadhalika amesema mwaka 1996, Tume ya Rais kuhusu Hali ya Rushwa iliwasilisha Taarifa yake iliyotambua rushwa kama Kansa inayohitaji kudhibitiwa ambayo isipodhitiwa, itapindisha na kuvuruga demokrasia, itavuruga utawala wa sheria na uhuru wa Mahakama.

Pia amesema kuwa kila kiongozi, mtumishi, mwananchi na wadau wote tuna wajibu wa kupinga na kukataa kila aina ya uovu katika jamii ikiwemo rushwa, uonevu, wizi, ubadhirifu wa mali na uvunjifu wa haki za binadamu.

Wananchi tunawajibika kuisaidia Serikali kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa wachache wanaotumia madaraka na nafasi zao vibaya, kupendelea au kuwaonea watu, kupokea rushwa, kutumia mali ya umma kwa maslahi yao binafsi n.k. Kutotekelezwa kwa wajibu huo kunafanya uovu uendelee kushamiri katika jamii na sisi kuwa sehemu ya uovu huo. Tusikubali kuwa sehemu ya tatizo bali tuwe sehemu ya suluhu ya tatizo. Inawezekana ikiwa kila mmoja akatimiza wajibu wake

Amesema ahadi ya uadilifu kwa sekta binafsi inawataka watumishi wa sekta hiyo kushiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa Taifa kwa njia ya kulipa kodi kutokana na shughuli zote za kibiashara kwa njia ya uwazi na uadilifu, kutoshawishi, kuomba, kupokea au kutoa hongo au aina yoyote ile ya rushwa.

Aidha, kuhakikisha kuwa mfumo wa kutoa taarifa za mapato ni wa uwazi na kutoruhusu kamwe vitendo vya rushwa na utovu wa maadili katika ununuzi wa umma.

Huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema serikali itaendelea kusimamia maadili na haki za binadamu kwa watumishi wanaoenda kinyume na masuala hayo na kutembea katika maadili potofu kwa kutozingatia utawala bora.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amesema wanalaani vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na kwamba serikali haina huruma na watu wanaofanya hivyo na kwenye hilo hakuna sehemu ya kuponea na badala yake watachukuliwa hatua stahiki.

 

Post a Comment

0 Comments