WAZAZI WASHAURIWA KUZINGATIA LISHE KWA WATOTO

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA 

MKURUGENZI Mkuu wa Diamanda Foundation, Diamanda Kaphipa amewaasa wazazi kuzingatia lishe kwa watoto shuleni na nyumbani ili kuondoa ukatili wa lishe kwa watoto.

Kaphipa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa hafla ya kutoa uji wa lishe kwa watoto kuanzia darasa la awali hadi darasa la nne katika shule ya msingi Makulu.

Leo tumekuja kwa ajili ya kutoa elimu kwa wazazi kuhusu lishe kwa watoto hasa shuleni, lakini pia tumekuja na uji wa lishe bora na wenye virutubisho vyote ili wazazi nao waige mfano huo.

Kaphipa

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Lishe bora na huduma zingine za msingi kama elimu na afya ni haki ya kila mtoto ikimaanisha kuwa watoto wote wana haki ya kupata elimu pamoja na lishe bora yenye virutubisho ili kusaidia ukuaji wa mwili, kiakili, kuondokana na udumavu unaotokana na lishe duni na hatimaye kufikia katika utimilifu wake.

Kwa maboresho yaliyoonekana kwenye taratibu za lishe kwa watoto wachanga na watoto wengine wadogo ni pamoja na unyonyeshaji na lishe ya vyakula vya ziada kuwa ni sababu muhimu zilizochangia katika kupunguza kiwango cha udumavu kitaifa kutoka asilimia 34.7 mnamo mwaka 2015 hadi 2016 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018.

Hata hivyo licha ya maboresho hayo ni muhimu kutambua kuwa udumavu mkali bado unaathiri mtoto mmoja kati ya watoto kumi nchini kote, hii inamaanisha kwenye kila watoto kumi wa umri chini ya miaka mitano, mtoto mmoja anaripotiwa kuwa na udumavu mkali ambapo inaashiria kwamba watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Tanzania wamedumaa.

Kaphipa amesema, kuna idadi kubwa ya watoto hukosa haki hususani lishe bora kutokana na sababu mbalimbali za familia ukiwemo umasikini wa kipato hali ambayo husababisha watoto kutopenda shule, kufanyiwa vitendo vya ukatili, kuwa na ufaulu mdogo darasani, kupata magonjwa ya mara kwa mara na kusababisha utapia mlo.

Mtoto akiwa na njaa anakuwa dhaifu hawezi akasoma kwa ufanisi kutokana na kukosa lishe inapelekea mahudhurio yake shuleni kuwa hafifu, lishe bora inajenga afya na akili, hivyo watoto wakipata  chakula shuleni na asubuhi kabla hajaenda shuleni itapunguza utoro shuleni lakini pia itapunguza vitendo vya ukatili.

Kaphipa

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema, wazazi wanakosea kutumia muda mwingi kutafuta maisha huku malezi ya watoto wakiyaweka kando hali inayosababisha changamoto nyingi kwa mtoto na hivyo kushindwa kufikia ukuaji timilifu.

Suala la ulezi ni jukumu muhimu na suala la utafutaji linafuata, lakini siku hizi wazazi wameweka mbele zaidi suala la kutafuta pesa, wamewasahau watoto na kuwaacha na wasichana wa kazi ambao hawana uelewa wowote kuhusu suala la lishe ya mtoto na hivyo kuwasababishia ukatili wa kukosa lishe bora. 
Kimweri

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa Makulu Anthony John Mkazi wa Makulu amesema, elimu waliyoipata kuhusu lishe kutoka kwa Diamanda Foundation imewafumbua macho huku akionyesha utayari wa kuhakikisha anazingatia suala hilo kwa watoto nyumbani pamoja na shuleni.

 

Post a Comment

0 Comments