MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 18 Januari 2023 ameweka Jiwe la Msingi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo eneo la Mwawaza kata ya Negezi katika Manispaa ya Shinyanga iliyogharimu shilingi bilioni 9.5 mpaka sasa.

Akihutubia viongozi, watumishi wa Hospitali pamoja na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga waliojitokeza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema ujenzi wa Hospitali hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya Serikali kuboresha na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi. Ameongeza kwamba kuwekwa kwa vifaa tiba kama vile CT- Scan katika Hospitali hiyo kuna lengo la kupunguza adha ya kusafiiri kwenda katika hospitali za mbali kama vile Bugando na Muhimbili ili kupata huduma hiyo.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa uongozi wa Wizara ya Afya, Mkoa wa Shinyanga, wataalam, wauguzi pamoja na wananchi wote kwa ujumla kutunza vyema majengo na vifaa tiba vilivyopo hospitalini hapo.

Makamu wa Rais amesema serikali itapeleka shilingi bilioni sita katika Hospitali hiyo ili iweze kukamilisha ujenzi wa jingo maabara pamoja na jengo la Mama na Mtoto. Vilivile serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya kilometa tano kuingia Hospitalini hapo kwa kiwango cha lami ambapo tayari shilingi Bilioni saba zimetolewa.

Hali kadhalika Makamu wa Rais ameiagiza TAKUKURU kuweka mkazo katika vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha watumishi wanaowadai wananchi rushwa wanashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria. Pia ameagiza vyombo vya dola kufuatilia na kuwabaini watu wote wanaofanya wizi wa dawa katika Mahospitali na Vituo vya Afya.

Vilevile amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakikisha Madirisha ya Wazee katika Hospitali yanafanya kazi na pia kuhakikisha huduma za dawa kwa wazee zinatolewa ipasavyo.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya kifua kikuu na kutumia dawa kwa usahihi kwa wale wenye maambukizi. Amiagiza Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Wizara ya Afya kuhakikisha sheria na kanuni za afya na usalama mahala pa kazi ikiwemo migodini zinafuatwa.

Pia amewaasa kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa migodi na wachimbaji kuhusu namna bora ya kujikinga na vumbi wanapokuwa katika shughuli za uchimbaji wa madini kwasababu vumbi la migodini ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa huo wa kifua kikuu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Mkoa wa Shinyanga umeokoa jumla ya shilingi milioni 403 katika kusafirisha wagonjwa kwa mwaka baada ya kuwekwa kwa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo ikiwemo X- Ray pamoja na CT-Scan.



Post a Comment

0 Comments