MKENDA:TUNATAMBUA MCHANGO WA SHULE BINAFSI HAPA NCHINI.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na shule binafsi katika kuinua na kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.

Ameyasema hayo leo Januari 21, 2023 Jijini Dodoma wakati wa kikao na wamiliki wa shule binafsi kilichohudhuriwa pia na viongozi wa idara mbalimbali zilizopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Niwatoe wasiwasi kuwa Serikali inatambua na inathamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini hivyo msifikirie kwamba tumewaacha nyuma hapana tunawahitaji sana muendelee kuwekeza katika Elimu yetu

Prof.Mkenda.

Aidha kati ya changamoto zilizotolewa na wamiliki wa shule binafsi ni kumuomba Prof.Mkenda kuvifungulia vile vituo vilivyosimamishwa kufanya mitihani na kuwachukulia hatua waliyohusika katika wizi wa mitihani badala ya kuzifungia shule kwani inadhorotesha maendeleo ya shule husika.

Prof.Mkenda amewahakikishia kulifanyia kazi suala hilo na kubainisha kuwa wapo katika hatua ya kuwapata wahusika kwa majina hivyo baada ya hapo Serikali kupitia Wizara ya elimu itatangaza maamuzi mengine juu ya vituo hivyo.

Kuna shule zimefungwa kuwa vituo vya mitihani, hatua tuliopo kwa sasa ni kuyapata majina ya waliyohusika katika wizi wa mitihani hiyo ni lazima wajulikane na wachukuliwe hatua kali za kisheria na hapa nasema hatapona hata mmoja atakayethibitika kuwa ameshiriki. Hii nasema kuanzia msimamizi wa mtihani mpaka yule mlinzi aliyekuwa analinda mtihani naye lazima achunguzwe ili kumpata mhusika halisi

Prof. Mkenda

Aidha, Prof. Mkenda amewataka wamiliki hao wa shule binafsi kusimamia malezi kwa wanafunzi katika shule zao ili kuendelea kutoa kizazi chenye maadili na kuondokana na matukio mabaya yanayoripotiwa katika baadhi ya shule kuwa kuna mafundisho yanayotolewa ya kinyume na maadili.

Pamoja na hayo Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali haiwezi kuwapangia kiwango cha ada shule binafsi kwa kuwa ni maamuzi ya mzazi/mlezi kupeleka watoto wake katika shule aitakayo.

Hakuna siku mtasikia Serikali inawapangia ada kwani ni uhuru wa mzazi kumpeleka au kutompeleka mwanae shule binafsi, ila huku Serikalini Elimu ni bure na hatuzuii kila mtu kuwa na chaguo lake ampeleke mwanae shule binafsi au Serikalini hapo sisi hatuingilii ili mradi mtoto aende shule

Prof. Mkenda

Kwa upande wao Wamiliki wa Shule binafsi wamemuomba Prof. Mkenda katika bajeti ya Wizara ijayo kuongeza bajeti ya kuwalipa idara ya uthibiti ubora wa shule wakati wanakwenda kutekeleza jukumu la kukagua shule kwani imekuwa ikiwaumiza kulipa ili waende kukaguliwa.

Pia wamiliki hao wameomba kuondolewa kwa gharama za Mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi kwani hawana tofauti na wanafunzi wanaosoma shule za Serikali ambao wao wamefutiwa gharama za mitihani.

 

Post a Comment

0 Comments