SENYAMULE AHIMIZA BALOZI KUJENGA DODOMA

 📌MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema mpaka sasa Balozi tatu (3) za Uganda, Zimbambwe na Zambia zimeanza ujenzi wa majengo ya Balozi hizo Mkoani Dodoma.

Ameyasema hayo leo tarehe 28/02/2023 mara baada ya kukutana na balozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Elisabeth Jacobsen aliembatana na ujumbe wake katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kutembelea Mkoa wa Dodoma.

Mhe. Senyamule amemshukuru Balozi wa Norway kwa kutembelea Dodoma, kuona fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili pia hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika kuifaharisha Dodoma.

Tunawakaribisha sana Dodoma, makao makuu ya nchi yetu, viwanja 67 vimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi na makazi ya balozi mbalimbali

Senyamule

Ameongeza kwa kusema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ili Dodoma iweze kufunguka kimataifa.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja ujenzi wa barabara za mzunguko, ndani na nje ya Mkoa pamoja na ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato.

Naye Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Balozi Elisabeth Jacobsen amesema kwa miaka mitano aliyokaa Tanzania ameshuhudia mageuzi na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi kifupi na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa vitendo agenda ya maendeleo endelevu.

Amesema kwa kipindi cha miaka miwili Mkoa wa Dodoma umebadilika sana kutokana na uwekezaji uliofanyika katika sekta ya miundombinu, Elimu, Afya na mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja ujenzi wa mji wa Serikali.

Balozi Elisabeth katika ziara yake ameambatana na ujumbe wa watu 21 na wanatembelea Mji wa Serikali Mtumba, Hospitali ya Benjamin Mpaka, Ujenzi wa Reli ya Kisasa na ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Msalato.

Aidha, Mratibu wa kikosi kazi cha Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshach Bandawe amesema ujio wa Balozi wa Norway ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali kuhamia Dodoma hususani kuhamasisha ujenzi wa ofisi za ubalozi na mashirika ya kitaifa.

 


Post a Comment

0 Comments