MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA(TRA)YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WAKURUGENZI WATATU KWA MAKOSA YA KUTENGENEZA RISITI BANDIA ZA KIELETRONIKI

 📌JASMINE SHAMWEPU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Dodoma imewafikisha mahakamani  Wakurugenzi Watatu wa Kampuni ya Corsyne Consult Limited kwa makosa matatu ya kikodi ikiwemo kutengeneza risiti bandia za kielektroniki na kuisababishia serikali hasara ya sh.milioni 100.7. 

Makosa mengine ni ulipaji wa kodi na matumizi yasiyo halali ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki.

Akizungumza na wandishi wa habari  jijini hapa, Ofisa Sheria wa TRA Mkoa wa Dodoma, Erasto Mtondokoso amesema washitakiwa  hao walitenda makosa kati ya Julai hadi Disemba mwaka jana na kufanikiwa kutengeneza risiti bandia  22 za vifaa vya ujenzi.

Kimsingi kwa makosa hayo matatuwashtakiwa wameisababishia hasara serikali sh.milioni 100.7. Kwa leo tumefanikiwa kumsomea shtaka mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo na Mkazi wa Mwanza Biswalo Peter Biswalo (38) ambaye hajakiri kutenda kosa hilo

Kwa mujibu wa Wakili Tondokoso amesema washtakiwa wengine watasomewa mashtaka Aprili 6 mwaka huu.

Amewataja washtakiwa wengine kuwa ni Denisi Kisoka (38) na Ezekieli Mayunga ambao wote ni wakazi wa Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake Meneja wa Idara ya Upelelezi wa Kodi Kanda ya Kati Nicholous Njovu amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakitengeneza risiti bandia ili kukwepa kulipa kodi.

Amewaataka wafanyabiashara wanaohujumu serikali kwa kutoa risiti bandia kuwa TRA wako macho na imeimarisha mifumo yake kuhakikisha inawanasa watuhumiwa wote wanaokwepesha mapato ya serikali

Natoa rai kwa wote waliokuwa na mpango wa kutengeneza risiti bandia waache mara moja, na wananchi wanatakiwa kudai risiti za kielekroniki pindi wanapofanya manunuzi

Aidha Njovu amewataka wananchi kuhakiki risiti wanazopewa kama ni halisi au bandia kwa kutumia simu zao za mkononi ama kufika katika ofisi za TRA kuuliza.

Ofisi zetu ziko wazi muda wote, kama mwananchi ana wasiwasi na risiti aliyopewa anaruhusiwa kuja kuuliza lakini pia anaweza kuangalia kupitia simu yake ya mkononi kwa wale wanaomiliki smart phone

 

Post a Comment

0 Comments