MIRADI YOTE IKAMILIKE KWA WAKATI - GUGU

📌 MWANDISHI WETU

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu amesema lengo na matarijio  ya Mkoa ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia muda uliowekwa na viwango vya ubora unaotakiwa kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Gugu ameyasema hayo leo tarehe 14/04/2023 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika Wilaya ya Bahi kwa lengo la kukagua utekezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Gugu amehimiza watumishi wanaosimamia miradi hiyo kuwajibika na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa miradi yote ya maendeleo na kutoa angalizo juu ya hatua zitakazochukuliwa dhidi ya miradi ambayo haitakamika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya afya na elimu katika Halmashauri zetu, tusiwe moja ya vikwazo katika kusimamia ukamilifu wa miradi hii, tunayotaka kufanya yafanyike kwa wakati na hapa nisisitize kubwa zaidi kusiwe na viporo vya kutokamilika kwa miradi ya maendeleo. Sote tudhamirie kukamilisha kazi zote zilizopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha kwa kuzingatia mpango kazi

 Gugu 

Awali, Katibu Tawala Bw. Gugu alipata wasaa wa kuzungumza na Watumishi wa Wilaya ya Bahi na kuwataka kutumiza wajibu wao kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Haki zinaenda sambamba na wajibu, hivyo timizeni wajibu wenu kikamilifu kila mmoja katika nafasi yake

Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iko katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa majengo 18 kati ya majengo 28 yanayotakiwa kwenye hospitali ya Wilaya ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 4.3 zimetumika.

Kutokana na kukamilika kwa baadhi ya majengo katika Hospitali hiyo imewezesha kuanzishwa kwa huduma ya mionzi, huduma ya upasuaji ambapo mpaka sasa akina mama 212 wamefanyiwa upasuaji, uwepo wa huduma za X-Ray na Ultrasound na kutoa huduma kwa watoto waliozaliwa chini ya umri kamili wa mimba yaani Watoto njiti.

Bw. Gugu katika ziara yake amekagua pia ujenzi wa Zahanati ya Nagulo, Shule ya Msingi Bahi English Medium Pre and Primary School, Shule ya Msingi Mpamantwa Barabarani na Shule ya Msingi Kigwe yenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.



Post a Comment

0 Comments