BILIONI 5.6 KUKAMILISHA SKIMU YA UMWAGILIAJI BAHI

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

SERIKALI imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo, Kata ya Babayu, Tarafa ya Mundemu yenye ukubwa wa hekta 220.

Hayo yamebainishwa leo na Bw. Raphael Laizer Meneja wa Mradi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa ujenzi wa bwawa hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, katika eneo la mradi.

Bw. Laizer amesema ujenzi wa skimu hiyo unaendelea na uko katika hatua za awali chini ya mkandarasi wa Kampuni ya M/S CRJE (EA) kutoka China.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa skimu hiyo ya umwagiliaji, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa na kilimo cha kisasa kwa kulima mara mbili mpaka tatu kwa mwaka, kuhamasisha shughuli za uvuvi na mifugo bila kuathiri mazingira.

Kilimo cha uhakika duniani kote ni kilimo cha umwagiliaji, kilimo kinachowezesha wananchi kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka

 Senyamule

Amesema maono ya Serikali ni kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi nyingine duniani katika kulisha dunia kwa kusambaza chakula ndani na nje ya nchi.

Amesema sababu za Serikali kuajiri maafisa ugani, kununua vitendea kazi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa pikipiki, kuimarisha vitalu vya mbegu zote ni nyenzo za kuimarisha usalama wa chakula na kuimarisha sekta ya kilimo.

Nae Bi. Francisca Ntizi amesema kukamilika kwa skimu hiyo ya umwagiliaji itakuwa ni fursa hususani ya kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato ikiwa ni pamoja kujihusisha na kilimo zaidi ya mara mbili kwa mwaka, uvuvi na kilimo cha mbogamboga.

Ujenzi huu wa skimu ya umwagiliaji umeanza Aprili 2023 na utakamilika baada ya miezi 18 ambapo pia rambo litajengwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.



Post a Comment

0 Comments