SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 2.7 KWA AJILI YA HUDUMA YA UPANDIKIZAJI ULOTO


📌JASMINE SHAMWEPU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu hayo kwa wananchi. Majaliwa amezindua huduma hiyo leo ambayo Tanzania itakuwa ya kwanza katika Ukanda wa nchi za Mashariki na kati huku ikiwa ya saba kwa nchi za Afrika.

Kwa lugha nyingine, kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi. Kwa mfano, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa katika hospitali hii, itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja

Amesema hayo leo  wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kuzindua huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) hasa kwa watu wenye Selimundu (Sickle Cell).

Waziri Mkuu amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuzindua huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto na hivyo, kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa selimundu kwani huwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu. Kutokana na nafuu hiyo, mgonjwa huweza kuishi maisha yenye ubora na kushiriki vema katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo

Amesema uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya.

Huduma za namna hii kuendelea kutolewa katika hospitali zetu si jambo dogo, na hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa huduma kama hizi zinapatikana katika nchi chache sana kwenye bara la Afrika.

Kwa Upande wake  Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kila mwaka duniani kote watoto wapatao 300,000 wanazaliwa na tatizo la Selimundu na hapa Tanzania kila mwaka wanazaliwa watoto 11,000 ambapo kati yao watoto 6,000 wanafikiwa na huduma za kliniki.

Watoto wanaozaliwa na tatizo la selimundu huwa wanapata maumivu ya mara kwa mara ya viungo, wanakuwa na tatizo la kupungukiwa damu, wanakosa masomo kwa miezi mingi. Kuna mzazi amesema mwanaye alikuwa anahudhuria masomo kwa miezi mitatu tu kati ya 10 anayopaswa kuwepo shuleni,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amesema Wizara hiyo inaangalia uwezekano wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ili iwe hospitali ya Taifa badala ya kuendelea kubakia kuwa ya kanda.

Tumeanza kujenga kituo cha kutoa tiba ya kansa na pia tunataka tujenge kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo ili kuimarisha utoaji wa huduma kwenye hospitali yetu.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika alimweleza Waziri Mkuu kwamba tangu Januari 19, mwaka huu hadi leo, wamefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto watatu na wote wanaendelea vizuri.

Watoto wawili wanatoka kijiji jirani cha Mapinduzi na mmoja anatoka eneo la Area D hapahapa Dodoma. Haduma hii  itasaidia nchi kupunguza idadi ya wananchi wanaoishi na selimundu ambao asilimia 50 hadi 90 huwa katika hatari ya kufariki kabla kutimiza miaka mitano

Dk Chandika

Chandika amesema Tanzania inakabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ambapo inashika nafasi ya nne Duniani na takriban watoto 11000 huzaliwa na ugonjwa wa selimundu Kila mwaka.

Ameseema kufanyika kwa upandikizaji wa uloto kwenye hospitali hiyo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika. Alizitaja nchi nyingine zinazotoa huduma hiyo kuwa ni Algeria, Afrika ya Kusini, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia.

 

Post a Comment

0 Comments