M-KAMERUN ALIYEMTIKISA FERGUSON •

 📌CARLOS CLAUDIO

ZILIKUWA nyakati ngumu kwa Sir. Alex Ferguson wakati akiwaza mrithi wa Roy Keane ambaye alikuwa mchezaji mtata na mwenye makeke mengi kwenye dimba la kati la Manchester United.

Katika mchakato wa kumpata kiungo mkabaji halisi alijikuta akimsajili Sebastian Veron lakini alishindwa kumshawishi na kumuuza Chelsea na yale mawazo yakaendelea kuisumbua akili yake.

Wakati wa michuano mikubwa ya Africa Cup Of Nations ya mwaka 2003 jicho la mpelelezi wa Ferguson lilitupia ndoano katika talanta za waafrika hatimae likainasa sura ya gwiji la Kamerun. Unamjua ni nani?

Alikuwa Eric- Daniel Djemba Djemba Kiungo mkabaji mwenye uwezo mkubwa wa kutembea na mpira eneo la kati, Djemba aliituliza akili ya Sir Alex Ferguson kwa ule uwezo wake. Wakati huo alikuwa akiitumikia Nantes ya nchini Ufaransa.

Ferguson bila kupepesa macho aliweza kumsajili Eric Djemba wakati huo Roy Keane akielekea ukingoni mwa soka lake, zilikuwa zama za Cristiano Dos Santos Ronaldo na kipaji chake bado unaongezewa Eric Djemba na mpira wake.

Kumhusudu sana kijana wake Ferguson akampa mshahara mkubwa Djemba ili kuipandisha thamani na morali ndani ya klabu, ila kilichotokea Djemba aligeuka kuwa mtu wa starehe, kila mwisho wa wiki akipokea mshahara kijana huyo alikuwa anashusha gari mpya na kukesha katika kumbi za starehe kitu ambacho kilimfanya kuwa na wakati mgumu kupata namba kikosini.

Tukio lile lilimkera sana Ferguson na kusema tatizo lilikuwa kumpa Djemba mshahara mkubwa, alidhani anamjenga kumbe anabomoa maisha yake. Baadae alimuuza katika klabu ya Aston Villa sehemu ambayo hakudumu na kuishia kutimkia Burnley kwa mkopo wa miezi sita kisha kufungasha virago na kukimbilia Qatar.

Huyo ndiyo Djemba Mkameruni wa kwanza kucheza Manchester United, Onana ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili na golikipa wa kwanza kutokea bara la Afrika kuidakia United. Amesajiliwa na kocha Eric Ten Hag kwa kitita cha Euro 47.2 milioni ikikadiliwa kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 148 za Kitanzania akitokea katika klabu ya Inter Milan iliyo na masikani yake jiji la Milan nchini Italia.

Kipa huyo anapaswa kuikwepa kasumba ya Eric Djemba na kuendeleza kipaji chake, Djemba baadae alisema anayajutia sana maisha ya jiji la Manchester, kwakua ni kijana masikini aliyeishi kitajiri katika jiji maarufu na la gharama na hatimaye kuendekeza starehe na kukatiza kipaji pamoja na ndoto zake.

Post a Comment

0 Comments