WILAYA AMBAZO HAZIJAFANYA UCHANGUZI HAZITASHIRKI UCHAGUZI WA KANDA NA TAIFA-MWENYEKITI CCWT

📌ABDULKARIM KESSY 

CHAMA Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimetoa tamko kwa wagombea wote wa chama ambao wamekidhi vigezo vya ugombea kuelekea uchaguzi mkuu wa chama hiko ili kuepusha vikwazo vitakavyojitokeza wakati wa uchaguzi huo wa mwaka 2024.

Hayo yameelezwa Machi 12, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chama Cha Wafugaji Bw. Charles Malanywa alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi ya chama ambapo amesema tangu mwaka jana wameanza mchakato wa uchaguzi na hadi sasa wanaendelea na chaguzi za ngazi mbalimbali ikiwemo za wilaya.

Malanywa amesema kuwa anawatangazia wafugaji na wanachama wote kuwa fomu za kugombea uongozi ndani ya chama, ngazi ya kanda na taifa zinaanza kutolewa tarehe 13, Machi hadi tarehe 25, Machi 2024 na mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi yeyote ya kanda anapaswa kuzingatia ratiba na kalenda nzima inayotolewa na tume.

Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi ili kuepuka mikanganyiko na hasa tunapotoa hii ratiba isije kuonekana kuna watu wana ratiba zao binafsi na hii ndio ratiba ya tume ya uchaguzi na sisi tunasema hiyo tarehe 13 kwa maana ya kesho  hadi tarehe 25, Machi tunaanza kutoa hizo fomu za kanda sambamba na fomu za ngazi ya taifa

Kalanywa.

Aidha, mwenyekiti huyo amesema vikao vya uteuzi ngazi ya kanda vitaanza kufanyika tarehe 21 na 23, Machi 2024 kama kutakuwa na watu wenye vipingamizi watasikilizwa na kutolewa maamuzi na baada ya hapo kutakuwa na ratiba ya uchaguzi kuanzia tarehe 25 hadi 30 Machi kwa ngazi ya kanda 8 zikiwa kanda ya juu kusini, Kusini, Mashariki, Kati, Kaskazini, Nyanza na kanda ya ziwa huku uchaguzi huo ukisimamiwa na wajumbe wa tume.

Malanywa amesisitiza kwa wagombea wote kufuata ratiba ya tume ipasavyo na kuchukua fomu kwa wakati kwani kwa ngazi ya taifa uchaguzi utaanza tarehe 8, Aprili 2024 ikiwahusu viongozi wote wa wilaya kuendelea kufanya uchaguzi wa ngazi za wilaya kabla haijafikia uchaguzi wa ngazi ya kanda kwani wilaya ambayo haitakuwa imefanya uchaguzi wa ngazi ya wilaya haitaruhusiwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya kanda pamoja na taifa kwasababu watakuwa hawajatimiza takwa la katiba ya wanachama.

Kwa upande wake mjumbe wa tume ya uchaguzi George Kituliko amesisitiza kwa wagombea na wanachama wote kuzingatia ratiba na tarehe husika ili kuepusha vikwazo vitakavyojitokeza kutokana na uzembe wa kufuata ratiba iliyotolewa na tume ya uchaguzi pia ameongeza kwa kusema wagombea wote watakaokuwa wanachukua fomu kwa ngazi ya kanda malipo yatafanyika katika akaunti ya tume na sio kukabidhi pesa kwa mjumbe yeyote, na baada ya malipo wahakikishe wanakuwa na stakabadhi ya malipo kutoka benki.

 

Post a Comment

0 Comments