📌 BAHATI MSANJILA
BENKI ya NMB imesaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati (MoU) wa miaka mitatu na Taasisi ya Tanzania Startup Association (TSA), yanayolenga kusaidia sekta ya wajasiliamali wachanga, kupitia bunifu za TeKnolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), zenye kuleta masuluhisho mbalimbali kwenye jamii.
Makubaliano
hayo ni muendelezo wa NMB katika kutilia mkazo na kujikita kwenye uwekezaji wa
kimkakati, ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuchochea ukuaji wa
biashara ndogo na za kati hasa zilizoko kwenye Sekta ya Sayansi na
Teknolojia.
Akizungumza
wakati wa kusaini makubaliano hayo, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Mabadiliko ya
Kidijitali wa NMB, Kwame Makundi, amesema dhamira yao ni kuhakikisha
wanaendelea kuwa mdau kinara wa kuchochea ukuaji wa biashara zenye mchango kwa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa na bara zima la Afrika.
Amesema kwa makubaliano
waliyoyasaini, ndani ya miaka mitatu NMB na TSA kwa pamoja zitasaidia
kukua na kuhakikisha uhai wa Startups nchini Tanzania, pamoja na kuunda mtandao
imara wa wajasiriamali, wabunifu, wawekezaji na wadau ili kusukuma ajenda ya
kitaifa ya ubunifu na ujasiriamali.
Kwa
mujibu wa Makundi, taasisi hizo kwa pamoja zitawezesha mazingira sawa na yenye
manufaa kati ya Startups na NMB, kuchukua jukumu la kuwa mabalozi katika kukuza
Startups nchini, huku wakiamini makubaliano hayo yatakuwa chachu ya ukuaji wa biashara
changa zilizo kwenye Sekta ya Sayansi na Teknolojia
Kwa kupitia makubaliano haya, pamoja na mambo mengine NMB itatoa bidhaa za huduma za kifedha zinazolenga biashara zinazoanza na za ubunifu (Startups) ili kusaidia ukuaji wa biashara hizo. Hii itajumuisha mikopo ya biashara, suluhishi za malipo, na vitendea kazi ili kusaidia biashara hizi ndogo na za kibunifu.
NMB itawapa wabunifu taarifa ya changamoto zilizopo kwenye soko, ambazo zitaongoza wabunifu kutengeneza suluhishi zinazofaa kutatua changamboto hizi, hii itafanikiwa kupitia programu kama vile ‘hackathons’ pia kupitia programu za kiubunifu, na majadiliano baina ya taasisi hizi mbili,
Ameongeza
kwamba NMB itatoa msaada wa kifedha kwa TSA kulingana na maombi na kwa
kuzingatia idhini ya ndani ya benki na wa bajeti, pamoja na kutoa nafasi
kwa biashara zinazoanza na za kibunifu nafasi za kuonyesha bunifu zao.
Majukumu
mengine ya NMB katika makubaliano hayo ni pamoja na kutoa elimu ya fedha na
usimamizi wa biashara ili kuwasaidia kifedha na kukuza biashara na bunifu zao,
ambapo Makundi kwa niaba ya NMB aliahidi kwa Watanzania kuwa benki yake itabaki
mstari wa mbele katika ukuzaji wa biashara changa na za kibunifu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu
wa TSA, ameishukuru NMB kwa ushirikiano wa muda mrefu na kwamba kwao wao
wanayatazama makubaliano hayo kama urasmishaji tu wa mahusiano ya kimkakati
waliyoanza miaka kadhaa iliyopita.
NMB imekuwaa mshirika na mdau wetu wa uhakika, wamefanya vizuri kusapoti ikolojia ya ‘startups’ ambapo walikuwa benki ya kwanza Tanzania kutusapoti na wanachokifanya kupitia MoU hii kuthibitisha na kuendeleza mahusiano mema baina yetu.
Tunatarajia uwezeshaji mkubwa kutoka NMB hasa katika masuala ya elimu ya fedha na mitaji, kwani tafiti zinaonesha kuwa katika kila biashara 10 zinazoanza, saba kati ya hizo zinakufa ndani yam waka mmoja wa kwanza wa biashara hizo, changamoto ikiwa ni masuala ya fedha na mitaji kwa ujumla wake,
Ameongeza kuwa ushirikiano na NMB
katika kufanikisha elimu na mitaji kwa startups ni jambo jema, linaloenda
kuzipa biashara changa na za kibunifu uhakika wa maendeleo na ustawi, kupitia
usaidizi wa elimu, mitaji na makongamano kutoka kwa wadau wao NMB.
Ukiangalia orodha ya kampuni kubwa 10 duniani, saba kati ya hayo zina rekodi za kuanzia chini na kwamba takwimu zinaonesha kuwa kiasi cha zaidi ya Sh. Bil. 800 zimeingia Tanzania kama uwekezaji kwa ‘startups,’ hii maana yake ni sekta inayochangia mitaji na pesa za kigeni nchini,
0 Comments