KAMPENI YA ‘NIPENDEZESHE NISOME’ KULETA MWANGA KWA WATOTO 500 DODOMA

 ðŸ“ŒBAHATI MSANJILA

ZAIDI ya watoto 500 wenye mahitaji maalum mkoani Dodoma wanatarajiwa kunufaika na kampeni ya Nipendezeshe Nisome, iliyozinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri.

Kampeni hiyo inalenga kusaidia vifaa vya shule kwa watoto wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini ili kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo  Jijini Dodoma, Shekimweri amesisitiza kuwa licha ya juhudi kubwa za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, bado wapo watoto kutoka kaya masikini wanaoshindwa kuhudhuria shule kutokana na ukosefu wa vifaa vya msingi kama sare za shule, madaftari, na vitabu.

Hali hii inahitaji ushirikiano wa jamii kwa ujumla. Tunapaswa kujenga utamaduni wa kuwasaidia watoto wenye uhitaji ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kusoma na kufikia ndoto zake

Shekimweri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kampeni hiyo, Sonatah Nduka, kutoka Redio C Fm ya Dodoma, amesema kampeni hiyo imelenga kuwapatia watoto vifaa vya shule kama sare, madaftari, chakula, na vitabu kwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Kampeni hii inalenga kuwasaidia watoto 500 wenye uhitaji mkubwa kuhakikisha wanapata vifaa vya shule ili waweze kusoma kama wenzao. Tunahimiza wadau mbalimbali kushirikiana nasi ili kufanikisha lengo hili

Nduka.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, Amon Sebyiga, alieleza kuwa watoto 30 kutoka shule yake watanufaika na kampeni hiyo.

Ameongeza kuwa msaada huo utaleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi ambao hapo awali walikuwa wakikosa mahitaji ya msingi ya shule.

Kampeni ya Nipendezeshe Nisome ni ishara ya mshikamano wa kijamii na inalenga kutoa nafasi sawa kwa watoto wote kujifunza, bila kujali hali zao za kifamilia.

Wito umetolewa kwa wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha elimu inafikiwa na kila mtoto mkoani Dodoma.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments