SERIKALI YATOA MAAGIZO KWA NHIF KUHUSU BIMA YA AFYA KWA WOTE

 ðŸ“ŒBAHATI MSANJILA

WAZIRI wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa weledi na kuzingatia maelekezo yanayolenga kufanikisha mpango wa bima ya afya kwa wote nchini. 

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mifumo ya kidigitali na mpango wa Toto Afya kadi, Waziri amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za Bima ya afya kwa wananchi.

 

Kama taasisi, mnatakiwa kuhakikisha mnapanua wigo wa wanachama, kuongeza ubora wa huduma, na kuondoa changamoto zinazolalamikiwa na wananchi bila kuathiri uhai wa Mfuko. Pia hakikisheni mnatoa taarifa kwa wakati ili kuepusha usambazaji wa taarifa zisizo sahihi


Waziri.

 

Aidha, Waziri Mhagama amekemea vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama.

 

Tabia ya kutumia Mfuko kujipatia mapato yasiyo halali haivumiliki. NHIF ituletee ripoti ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wa vitendo hivi ili kulinda uhai wa Mfuko

 

Katika tukio hilo, NHIF imezindua mifumo ya kidigitali inayolenga kuboresha huduma kwa wanachama na watoa huduma. Mifumo hiyo inajumuisha Mfumo wa Usajili wa Wanachama, unaomwezesha mwananchi kujiunga na kujihudumia kupitia mtandao, Mfumo wa Uwasilishaji na Uchakataji wa Madai, ambao umeunganishwa na zaidi ya asilimia 80 ya vituo vya afya nchini.

 

Waziri Mhagama pia amezindua mpango wa TOTO Afya ulioboreshwa, ambao unaruhusu watoto kujiunga na bima kwa makundi au mmoja mmoja iwapo hawapo shuleni Mpango  unaolenga kupunguza gharama za matibabu kwa familia nyingi na kuwahamasisha wananchi kusajili watoto wao.


Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka amesema mifumo hiyo mipya, Mfumo wa Usajili wa Wanachama na Mfumo wa Uchakataji wa Madai imetengenezwa na wataalamu wa ndani kwa gharama nafuu ya Sh milioni 445, ikilinganishwa na Sh bilioni 3.5 ambazo zingetumika kwa wakandarasi wa nje.

 

Mifumo hii itarahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Mfuko. 

 

Mfumo wa usajili utawaruhusu wanachama kujihudumia wenyewe kupitia simu au mtandao bila kufika ofisini, huku mfumo wa uchakataji madai ukipunguza muda wa ulipaji wa madai kutoka siku 90 hadi wastani wa siku 45,” alisema Dkt. Isaka.

 

Akitoa tathmini ya utendaji wa NHIF, Dkt. Isaka amesema kuwa kati ya Julai 2023 na Oktoba 2024, Mfuko ulifanikiwa kusajili wanachama wapya 839,331 na kufikia jumla ya wanachama wachangiaji 1,359,772. Hii imesababisha ongezeko la wanufaika wa bima ya afya hadi milioni 5.1, sawa na asilimia 8.4 ya Watanzania wote.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, Mhe. Elibariki Kingu amesema ustahimilivu wa sekta ya afya na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni msingi wa kuimarisha amani na utulivu nchini.

 

Amesisitiza kuwa Bima ya afya ni muhimu kwa maisha ya kila Mtanzania, kwani inatoa uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu, jambo ambalo linaweza kupunguza msongo wa maisha kwa wananchi.

 

Mhe. Kingu ameishauri NHIF kuimarisha kitengo chake cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT) ili kuongeza uwezo wa kufuatilia na kudhibiti vitendo vya ubadhilifu kuanzia ngazi za chini na kueleza kuwa mifumo ya kisasa na ufuatiliaji wa karibu ni nyenzo muhimu za kuhakikisha uadilifu na ufanisi katika utendaji wa Mfuko huo.

 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa NHIF kuhakikisha bei za vifurushi vya Bima ya afya vinakuwa rafiki kwa hospitali zote, za umma na binafsi. AMEsema usawa huu wa gharama utasaidia kuboresha ushirikiano baina ya NHIF na watoa huduma za afya, hivyo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora popote walipo nchini. 

 

Uzinduzi wa mifumo hiyo na mpango wa Toto Afya Kadi unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na za haraka kwa wanachama wa NHIF, huku ukichochea ushirikishwaji wa wananchi wengi zaidi katika mfumo wa Bima ya afya nchini.

 



Post a Comment

0 Comments