SERIKALI ya Awamu ya Sita imeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya nishati baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Mashaka Biteko, kuzindua mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze (Pwani) na Zuzu (Dodoma).
Uzinduzi wa mradi huu unaashiria hatua kubwa katika kuhakikisha umeme unaozalishwa na Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unawafikia wananchi wote, pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi, viwanda, migodi, na usafirishaji wa umeme katika kanda za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Dkt. Biteko amesema kuwa mradi huu ni hatua kubwa ya kuimarisha miundombinu ya nishati nchini na kuhakikisha kuwa Tanzania inajitosheleza kwa umeme wa uhakika.
Mradi huu utaunganisha mikoa yote muhimu, ikiwa ni pamoja na Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Pia utaimarisha biashara ya umeme na kushirikiana na mataifa jirani katika usambazaji wa nishati
Aidha, alibainisha kuwa juhudi hizi za Serikali zimeiwezesha Tanzania kuongoza Afrika katika usambazaji wa umeme kwa wananchi, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.
Serikali imeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 3,169.26, huku mahitaji ya juu yakiwa megawati 1,888.72. Hii inatuweka katika nafasi bora ya kukuza uchumi na kuhudumia sekta zote muhimu za kiuchumi
Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya nishati na kutoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, kuhakikisha kuwa wahujumu wa miundombinu wanachukuliwa hatua kali.
Matukio ya hujuma ya miundombinu si tu yanapoteza rasilimali, bali pia yanarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya nishati. Hakuna huruma kwa wahusika
Kwa mujibu wa Dkt. Biteko, Oktoba na Novemba 2024 pekee, kulikuwa na matukio 23 ya uhalifu wa miundombinu ya nishati, huku kati ya Julai na Septemba, matukio 35 yaliripotiwa. Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wahalifu wanachukuliwa hatua kali.
Ni lazima tulinde miradi inayotekelezwa kwa gharama kubwa ili kuhakikisha huduma za nishati zinaimarika. Hatua madhubuti zitachukuliwa kwa yeyote anayeharibu miundombinu hii
Kwa upande wake, Waziri Bashungwa amesema kuwa Wizara yake itahakikisha usalama wa miundombinu yote ya nishati, huku akibainisha kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi kama hii.
Tutahakikisha wahalifu wanachukuliwa hatua mara moja. Miundombinu ya nishati ni rasilimali ya taifa na ni lazima ilindwe kwa nguvu zote
Akizungumza kuhusu mafanikio ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, amesema kuwa mradi wa Chalinze-Dodoma unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 513 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme umefikia asilimia 80.
Kukamilika kwa mradi huu kutaboresha zaidi sekta ya nishati kwa kuimarisha usafirishaji wa umeme kutoka JNHPP. Pia utaongeza fursa za kiuchumi katika maeneo mengi ya nchi
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema mradi huu unahitaji usimamizi na utunzaji bora ili kuhakikisha matunda yake yanaendelea kuwanufaisha Watanzania.
Tunaahidi kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa. Tunaishukuru Serikali kwa kuweka kipaumbele katika sekta ya nishati
Mradi wa usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma ni moja ya miradi mikubwa inayolenga kuimarisha sekta ya nishati na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini. Kupitia miradi kama hii, Tanzania inaendelea kujiimarisha kama taifa linalotegemewa katika sekta ya nishati barani Afrika.
0 Comments