📌BAHATI MSANJILA.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa chama
hicho kuhamasisha vijana kujijiandikisha kwenye daftari la Tume ya Uchaguzi ili
waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo jijini Dodoma,
katika kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya chama cha mapinduzi, yaliyofanyika
uwanja wa Jamhuri. Alisisitiza umuhimu wa kila mwanachama kujiandikisha kwenye
daftari la wapiga kura, akisema kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki ya
kupiga kura inatambulika.
“Vijana, tunahitaji kuhakikisha mnaingia kwenye
daftari la wapiga kura ili kushiriki kwenye uchaguzi. Bila ya kuwa kwenye
daftari, hatuwezi kupiga kura.
Hivyo, ni muhimu vijana wote wa Kitanzania waende
na kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura,” alisisitiza Dkt. Samia.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia alitaja kuwa CCM
inajivunia mafanikio ya chama, ikiwemo kuwa na zaidi ya wanachama milioni 12 na
wapenzi wengi, huku akieleza kuwa chama kimejipanga vema kuelekea uchaguzi mkuu
wa mwaka 2025.
“Chama cha Mapinduzi kina mtaji mkubwa unaotokana
na kukubalika kwake na utekelezaji mzuri wa ilani yetu. Tumekuwa na mafanikio
katika nyanja mbalimbali, na sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu tukiwa na
nguvu kubwa,” alisema.
Dkt. Samia pia aliwashukuru wanachama wa CCM kwa
imani yao, akieleza kuwa chama kitashinda uchaguzi wa 2025 kwa kushirikiana na
wananchi.
Akizungumza kuhusu vijana, Dkt. Samia alisema kuwa
ni muhimu kuwajengea uwezo wa kisiasa na kiitikadi, ili waweze kuimarisha
jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT) na jumuiya ya Wazazi. Alisisitiza umuhimu wa
kuwa na viongozi vijana ambao wangeimarisha chama katika ngazi zote.
Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi,
alifafanua kuwa sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya chama hicho zitaendelea
kufanyika kila baada ya miaka mitano, na mwaka huu sherehe hizo zilifanyika
kitaifa, zikihusisha mikoa mbalimbali. Alieleza kuwa kaulimbiu ya sherehe za
mwaka huu inasisitiza uadilifu katika uchaguzi na aliwataka wanachama wa CCM
kushiriki kwa uadilifu ili kuendeleza mafanikio ya chama.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam
Kimbisa, alitoa ahadi ya kushinda kwa kishindo uchaguzi wa 2025, akisema,
“Tunaahidi kuleta ushindi shindo hapa Dodoma,” na kuongeza kuwa wananchi wa
Dodoma wataunga mkono chama kwa nguvu zote.
Sherehe hizo zilijumuisha shughuli mbalimbali za
jumuiya za CCM na ziara za viongozi mbalimbali, na kilele chake kilifanyika
jijini Dodoma.
0 Comments