COSTECH INAVYOPAMBANIA UFUGAJI WA KISASA .


 



📌DOTTO KWILASA.

 Ni ukweli usiopingika kwamba  nchini Tanzani kuanzia wasomi na hata wale wasio na elimu ya darasani swala la kilimo cha malisho ya mifugo ni wimbo usioeleweka masikioni mwao.

Lakini je, tuache kuchukua njia sahihi kwa sababu ya ukosefu wa uelewa juu ya swala hili? Kilimo cha malisho ndio njia pekee ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kusaidia ufugaji wa kisasa kwa mategemeo ya kupata bidhaa bora. 

Uhakika wa malisho  ni njia itakayomwezesha na kumuhakikishia mfugaji uhakika wa chakula cha mifugo wakati wa kiangazi ambapo Mfugaji mwenye kuweza kudhubutu kulima malisho atakuwa na uwezo wa kuvuna na kuweka akiba ya malisho(kipindi cha msimu wa masika) na kutumia akiba hiyo kipindi cha kiangazi wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa malisho. 

Jukumu hili linabaki kwenye mamlaka husika kuhakikisha mbegu za malisho bora zinapatikana ili elimu ya kilimo malisho iambatane na mbegu za malisho.

Hata hivyo katika kipindi  ambacho mifugo mingi inakufa tusiwalaumu wafugaji kwa kuwaambia hawataki kuuza mifugo haswa msimu wa kiangazi wakati tunajua mapungufu ya soko letu la mifugo na mazao yake na wala hatupaswi kuwalaumu kutangatanga wakati tunajua hali ya machunga hapa nchini.

Tunachotakiwa kufanya,ni kukomboa ufugaji na ukaendelea kushamiri kwa wafugaji hawa hawa tunaowalaumu kwa kuhamasisha kilimo cha malisho kwa wafugaji na kutumia mashamba darasa kuelimishia wafugaji hakika kilio cha malisho msimu wa kiangazi tutakitokomeza.

 Hali hii itamsaidia Mfugaji kuvuna  nyasi na kuziandaa kwa ajili ya hei(HAY) baadae kuzifunga vizuri na kuzitunza hadi msimu wa kiangazi ambapo hakuna malisho kwa wingi,kama mfugaji atakuwa na uwezo wa kuvuna mara nne kwa mwaka, maana yake atakuwa na uwezo wa kuzalisha hay nyingi zaidi ili kuilinda mifugo yake msimu wa kiangazi isihangaike na chakula na kuwa bora kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Na kwa kuwa wafugaji wengi wa kitanzania ni wale wenye shughuli  asili ambazo kwa namna moja au nyingine huchochea uharibufu wa mazingira kutokana na kuhama hama,ufugaji huu wa kisasa utasaidi kuondoa migogoro mingi ya ardhi.

 Jamii za Wagogo, wasukuma na wamasai ndizo zimekuwa zikitajwa kama chanzo kikubwa cha mifugo na mazao ya mifugo katika masoko na minada yetu hapa nchini na nje ya nchi. 

Lakini kama ufugaji ndio utamaduni wao je, ni kweli tuna sababu ya kupoteza utamaduni huo? Jibu ni hapana,bali tunacho takiwa kufanya ni kusaidia kuboresha mfumo wa ufugaji kuhakikisha kuwa mfugaji anafaidika na ufugaji wake wa kila siku kwa ajili ya kuongeza kipato na kustawisha uchumi wa nchi.

Kwa umuhimu huo,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika kipindi cha miaka 10 (2010-2020) imewezesha miradi 100 ya utafiti na ubunifu ambayo inaendelea kuwanufaisha watanzania  katika kuwaongezea kipato kwa kutoa Bilioni 50 .

 COSTECH kwa kushirikiana na  baadhi ya vituo vya utafiti wa kuendeleza malisho ya mifugo (TALIRI) vya Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma wameona umuhimu wa kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa waandishi wa habari za Sayansi wa mikoa ya kanda ya Kati ili kuwafikishia wafugaji na jamii kwa ujumla .

 Kwa mujibu wa mtafiti wa malisho ya mifugo TALIRI –Kongwa George Fupi wafugaji wanapaswa kuendana na wakati kwa kufuga kisasa na kuondokna na ugugaji holela wa kuhama kutoka sehemu moja na kwenda nyingine kwani kunasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuleta migogoro ya wakulima na wafugaji.

 Mtaalamu huyo wa malisho anaeleza kuwa ili kuondokana na migongano hiyo,wafugaji wanapaswa kuzingatia kupanda  malisho ya mifugo kwa kuzingatia hali ya hewa ya sehemu husika.

 

Malisho ni chakula muhimu sana kwa mifugo, kwa kawaida mifugo hupata chakula hasa nyasi katika malisho ya asili,lakini chakula hiki hakitoshelezi mahitaji kwa kuwa  hakina viinilishe vya kutosha kwa afya bora ya mifugo Kwa mfano, kiasi cha protini na madini ni kidogo ukilinganisha na malisho ya kisasa,amesema Fupi

 

Fupi ameongeza kuwa,mambo makuu mawili kwa mfugaji wa kitanzania yanayomkuba ni mabadiliko ya tabia nchi linalotokana na ongezeko kubwa la watu ambalo linazidi kuimega ardhi ya malisho kwa shughuli mbalimbali kama makazi na kilimo.

 “Kuendana na hali hii ya mabadiliko kuna kila sababu ya mfugaji kuona sasa umuhimu wa kujikita katika kilimo cha malisho ya mifugo,hii ina maana kwamba mfugaji atatakiwa kununua ardhi na kujikita katika kilimo cha malisho ili kuhakikisha ustawi wa mifugo yake kwa mwaka mzima,”anafafanua mtaalamu huyo aliyebobea masuala ya malisho.

 Kwa upande wake Mtafiti na msimamizi wa idara ya shamba TALIRI-Mpwapwa Erick Mbisha anaeleza kuwa Kilimo malisho kinahitaji ushauri wa kitaalamu haswa kuweza kutambua aina ya majani yanayoweza kustahimili kulingana na eneo analopatikana mfugaji.

 “Ni kweli kuna gharama zake ,lakini faida yake ni kubwa zaidi kuliko kutangatanga na mifugo katika kipindi ambacho malisho hayapatikani,kilimo cha malisho kinampa mfugaji uwezo wa kuvuna nyasi hadi mara nne kwa mwaka na kujitengenezea uwezo mkubwa wa kuhudumia mifugo yake,”anasema na kuongeza;

 Kilimo cha malisho kitapunguza kutembeza mifugo umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kutafuta malisho jambo ambalo huharibu ubora wa nyama, hudhoofisha mifugo na kuipunguzia uwezo wa kuzaliana (reproductive efficiency),”anasisitiza Mbisha.

 Naye Daktari mtafiti wa mifugo kituo cha utafiti Mpwapwa Malongo Mwalingo alieleza kuwa Mahitaji makubwa ya mifugo ni malisho na maji na ndizo zimekuwa sababu za ufugaji wa kuhama hama wafugaji kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta mahitaji ya mifugo yao.

 Anaeleza kuwa katika uhamaji  ndipo yanapotokea   mapigano ya wafugaji na wakulima.

“Serikali imezidi kujitahidi kumaliza migogoro hii lakini imekuwa ikijirudia kwa sababu hakuna suluhisho la mahitaji ya mfugaji katika eneo lake kutokana na wafugaji wengi kutokuwa na uelewa wa malisho ya kisasa,’’anasisitiza.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa asilimia 60 ya eneo la ardhi hapa nchini ni mbuga za malisho ya asili ambayo hutegemewa kwa chakula na mamilioni ya mifugo na wanyama pori walakini malisho haya hukomaa na kukauka mapema zaidi na hivyo kusababisha lishe yake kuwa duni na ustawi hafifu kwa wanyama wanaoyatumia hususani nyakati za kiangazi .

Dk.Mwalingo anasema kutokana na upungufu wa ubora wa malisho haya, upo umuhimu wa kuotesha aina bora za malisho kwa kuzingatia Utayarishaji wa shamba, Kurutubisha ardhi na upandaji.

 “Katika utayarishaji wa Shamba endapo shamba lako lina miti au vichaka inabidikwanza lisafishwe ili kurahisisha ulimaji, Shamba laweza kusafishwa kwa kutumia moto, kufyeka na kung’oa au njia zote tatu kwa pamoja na baada ya kusafisha, kazi ni kulima na upandaji,”anafafanua.

 Pamoja na hayo anabainisha kuwa  ulimaji huo waweza kufanyika kwa kutumia jembe la mkono au plau ya ng’ombe au trekta. 

 “Mkulima anapaswa kuhakikisha amepiga harrow ili kulainisha udongo  kurahisisha uotaji wa mbegu za malisho ambazo nyingi huwa na umbo dogo,kurutubisha ardhi ni muhimu ili kurekebisha upungufu wa madini mbalimbali yanayohitajika na mimea,”anasema.

 Katika kufanya hivyo waweza kutumia Samadi, mboji au mbolea za chumvi chumvi ambapo upandaji wa mbegu za malisho yafaa kuzingatia ubora wa mbegu, wakati wa kupanda, na njia za kupanda.

Hata hivyo Mwalongo anasema ubora wa mbegu unapaswa kuzingatiwa kutokana na sehemu zinazoaminika kama vile Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Mabuki, vituo vya Utafiti wa Malisho ya Mifugo kama Kongwa na Mpwapwa (Dodoma).

 “Mbegu nyingi zinastawi kulingana na hali ya hewa ya eneo husika,kwa Mpwampwa na Kongwa mbegu za malisho zinazostawi ni pamoja na Panicum Maximum,Bothriochloa Inclupta,Cenchius ciliaris na Eragrostis superb,”anasema.

Mbegu hizi ziliunganishwa kati ya majani ya asili na mbegu kutoka Austrelia ambayo ina virutubisho vingi ambavyo licha ya kuhifadhi mazingira wanyama wengi pia wanaipenda. 

..................

 

Post a Comment

0 Comments