TAKUKURU YAWASHIKILIA WANAFUNZI 13 KWA TUHUMA ZA RUSHWA:




📌RAMADHAN HASSAN.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma inawashikilia wanafunzi 13 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) cha Jijini hapa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani.

Imedaiwa kwamba wanafunzi hao kwa  kutumia rushwa waliweza kurudia kufanya mtihani  nje ya chumba cha mtihani na baadae walijaribu kuingiza karatasi za kujibia  mtihani kwenye mfumo rasmi ambapo alidai Chuo kiliwabaini na kutoa taarifa Takukuru.

Hayo yameelezwa leo Januari 16 mwaka huu na  Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma Sostenes Kibwengo wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari juu  ya utendaji wa Takukuru Mkoa wa Dodoma kwa robo ya Oktoba hadi Desemba mwaka 2020.

Kibwengo amesema wanawashikilia wanafunzi hao wa mwaka wa tatu kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani marudio ( supplementary examination) wa somo la Applied Statistics II uliofanyika Novemba mwaka jana chuoni hapo.

Amesema uchunguzi wa awali umeonesha kwamba wanafunzi hao kwa kutumia rushwa waliweza kurudia kufanya mtihani huo  nje ya chumba cha mtihani na baadae walijaribu kuingiza karatasi za kujibia  mtihani kwenye mfumo rasmi ambapo alidai Chuo kiliwabaini na kutoa taarifa Takukuru.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Dodoma amewataka waliokuwa wanafunzi wa Chuo hicho,Evarist Nyaki na Lameck Kawinga kuripoti mara moja kwenye ofisi za Takukuru Mkoani Dodoma kwa ajili ya kusaidia uchunguzi huo.

Wakati huo huo,Takukuru Mkoa wa Dodoma wamemkamata Mtaalamu wa nyama, raia wa Kenya Alexander Mwikali (42) ambaye anaishi Nkuhungu Jijini hapa  kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 200,00 kwa Mganga Mkuu wa Serikali,Profesa Abel Makubi  kama kishawishi ili apatiwe cheti cha uthibitisho wa kutokuwa na ugonjwa wa Corona.

Aidha,Mkuu huyo wa Takukuru amesema Jumatatu,Takukuru Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka itamfikisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma,aliyekuwa Mhasibu Msaidizi Mapato wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Severo Mutegeki (42).

Kibwengo amesema Mutegeki atafunguliwa shauri la uhujumu uchumi ambapo atashtakiwa kwa makosa matatu ya matumizi mabaya ya Mamlaka ,ubadhilifu na kuisababishia Mamlaka hasara ya zaidi ya shilingi milioni 428 kinyume cha sharia ya uhujumu uchumi sura ya 200,marejeo ya mwaka 2019.

mwisho


 

Post a Comment

0 Comments