📌NA MWANDISHI WETU.
WAZIRI, wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji ambapo katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano ya Dk. John Pombe Joseph Magufuli uzalishaji wa sukari umeongezeka kwa 78.3 %(kutoka tani 295,775 mwaka 2015/2016 hadi tani 377,527 zinazotarajiwa kuzalishwa msimu wa 2020/2021).
Mafanikio haya ya kuongezeka kwa uzalishaji ni matokeo ya utekelezaji wa Sera na Mikakati ambayo Serikali imeweka kuhakikisha wazalishaji wana mazingira mazuri ya wazalishaji kufanya upanuzi wa mashamba na wakulima kuongeza tija.
Prof.Mkenda ameongeza kusema
Uzalishaji wa sukari kwa mwaka nchini ni wastani wa tani 300,000 ambapo katika msimu wa mwaka 2020/2021 jumla ya tani 377,527 za sukari zitazalishwa kutoka kwenye viwanda vilivyopo vya Kilombero Sugar Company Ltd, Mtibwa Sugar Estate, Kagera Sugar Ltd, TPC Ltd na Manyara Sugar Ltd.
" Kwa ujumla mahitaji ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida na viwandani ni tani 655,000 kwa mwaka, ambapo katika hizo tani 490,000 zikiwa na ziada (buffer stock) ya tani 70,000 sawa na mahitaji ya miezi miwili ni sukari ya matumizi ya kawaida na tani 165,000 ni matumizi ya viwandani" alilsitiza Prof .Mkenda
Waziri huyo wa Kilimo alisema Kutokana na uzalishaji huo , sukari inayozalishwa nchini haitoshelezi mahitaji ya soko la ndani na hivyo Nchi huagiza wastani wa tani 40,000 za sukari ya matumizi ya kawaida (Gap Sugar) kufidia pengo la mahitaji halisi ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida.
Prof. Mkenda alitaja mikakati ya kuongeza uzalishaji sukari kuwa ni kuwapatia wakulima mbegu bora ya miwa, kujenga miundombinu ya umwagiliaji na kuhakikisha viwanda vya sukari nchini vinachakata miwa yote inayovunwa na wakulima hapa nchini.
0 Comments