TANTRADE YATOA ONYO KWA WASIOFUATA SHERIA ZA MAONESHO



📌DEVOTHA SONGORWA. 

WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara  nchini wametakiwa kufuata sheria na taratibu za maonesho ya biashara bila shuruti kuepuka  malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wananchi ikiwemo kutapeliwa fedha zao.

 Akizungumza jana na mtandao huu Mwanasheria wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Fikiri Mboya amesema mamalka hiyo moja ya majukumu yake ni kudhibiti maonesho akisema baadhi ya watu hupeleka bidhaa zao katika maonesho bila kuwa na vibali akisema kwa atakayebianika   sheria itachukua mkondo wake.

 Amesema sheria namba nne ya mwaka 2009 ambayo ilianzisha mamlaka hiyo inawataka TANTRADE kutoa vibali kwa yeyote atakayetaka kufanya maonesho nchini huku akisema wapo baadhi ya watu wasiyo waaminifu hufungua maonesho bila kuomba kibali na kujiingizia  kipato kinyume cha sheria hali inayoharibu sifa ya mamlaka. 

“Kuna baadhi ya wananchi hawazingatii sheria watu wanalalamika kutapeliwa mtu anajitokeza tu anataka kufanya maonesho wananchi wanachangia fedha mwisho tunaulizwa sisi TANTRADE jambo hili mlilifanyaje sasa hii inaumiza wafanyabiashara niwasihi wananchi wafuatilie kwanza kama sisi tuna taarifa hizo kabla hujatoa pesa yako hatutamuonea mtu huruma endapo atabainika,”alisema Mwanasheria huyo.

 

Pia amewataka wafanyabiashara kutumia masoko ya ndani kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora hatua itakayosaidia kuongeza wigo wa masoko kimataifa akisema wengi wamekuwa wakilalamikia ufinyu wa masoko ya bidhaa zao kutokana na kuzalisha kwa mazoea na kukosa elimu ya biashara.

 Amesema yapo mataifa mengi Duniani ambayo yanahitaji bidha mbalimbali kutoka Tanzania na wao kama mamlaka husika wana wajibu wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya wafanyabiashara akisema wanachukua hatua  kuhakikisha yanapatikana ili watanzania kupeleka bidhaa zao.

 

“Kuna mahitaji makubwa ya bidhaa zetu katika nchi za wenzetu  kama matunda na nyinginezo tunawasiliana na balozi  mbalimbali na unakuta nchi husika wanasema vitu wanavyovitaka nasi tunafahamisha umma kwa wenye uwezo wanapeleka lakini bado wajasiriamali wengi wanazalisha  bidhaa chini ya viwango,”alisema Mwanasheria huyo.

 Akizungumzia fursa ya maonesho ya biashara ambayo hufanyika kila mwaka aliwataka wafanyabiashara kuacha uwoga wa kujitangaza na badala yake wajitokeze kushiriki kwani huwasaidia kukutana na wafanyabiashara wakubwa hivyo kuongeza ubunifu, kupata elimu,kubadilishana uzoefu na kujenga uhusiano wa kibiashara.

 “Tuwahimize wajasiriamali na wafanyabiashara tunaelekea katika maonesho ya biashara mwezi Juni 28 hadi 13 Julai niwaambie huo ni mwanya mzuri  unazalisha kitu fulani unakutana na mnunuzi na wanakuwa kutoka ndani na nje ya Tanzania pia unapata changamoto utakosolewa pale, utapewa mbinu mpya itakusaidia kuwa mzalishaji bora,”alieleza Mboya.

 Mwanasheria huyo alieleza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao hushirikiana na Wizara ya kilimo kujadili kwa pamoja namna ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao kuleta tija kwa kuwapatia kipato na kuongeza pato la Taifa.

 “Tunafanya kazi kwa kushirikiana na malaka zingine tunashughulika pia na kipengele cha utoaji wa elimu ya kuongeza thamani ya bidhaa sasa tunapokutana na wizara ya kilimo inakuwa rahisi kwetu kwani wao wako karibu zaidi na wakulima tunatamani kuona kila mkulima anafaidika na nguvu kazi yake,”alibainisha Mboya.

 Hata hivyo alieleza kwamba  Mamlaka hiyo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo baadhi ya majukumu yao ni utafiti wa masoko, kuwajengea uwezo na kuwaendelea wajasiriamali, kutoa huduma za ushauri kuhusu ushindani wa kibiashara, kuendeleza bidhaa na masoko pamoja udhibiti wa maonesho ya kimataifa ndani na nje  ya nchi na kushauri serikali katika sera na uwezeshaji.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments