WAKAZI WA WISIKWANTIS WALIOKOSA MAJI SAFI TANGU NCHI KUPATA UHURU.

 



📌RAMADHAN HASSAN.

 WAKAZI wa Kata ya Wisikwantis Wilayani Kondoa  Mkoani Dodoma wanalazimika kunywa maji ya kwenye madimbwi  kutokana na kutopata maji safi na salama tangu kupatikana kwa uhuru.

 Pia wamesema licha ya kuwa Mjini  lakini hakuna barabara za kuweza kufika katika eneo hilo pamoja na kukosekana kwa huduma ya  umeme hali ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu.

 Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo Februari 2 mwaka huu,Wakazi hao wamedai kwamba maisha kwao yamezidi kuwa magumu kutokana na kutopata huduma za kijamii kwa muda mrefu.

 Mohammed Soloka amesema kwamba licha ya kwamba wapo mjini lakini kwao huduma ya maji ya bomba  imekuwa mtihani mkubwa kwani tangu upatikane uhuru hawajawahi kuipata.

 Soloka amesema licha ya kupiga kelele na kupaza sauti hakuna ambeye amekuwa akiwasaidia huku wakazi wa eneo hilo wakichimba mashimo katika makorongo zaidi ya mita mbili ili kupata maji.

 “Wakati wa masika huwa afadhali kwani huwa tunachimba vishimo vidogo tunatoa yale maji  machafu tunachota masafi,kiangazi ni mchanga tu hili korongo linatoka  katika maeneo ya  Bolisa na  Ghubali lakini wakati wa kiangazi ni shida tupu tunachimba mpaka  mita mbili ndio tunapata maji,”amesema Soloka.  

 Kutokana na hali hiyo wameiomba Serikali iwasaidie ili waweze kupata maji ya bomba  kwani wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu.

 Pia, Soloka amesema licha ya maeneo ya jirani kuwa na umeme lakini wao wamekuwa wakiishi gizani ambapo amedai ni kama wametelekezwa huku wenye Mamlaka wakiwa kimya.

 “Mbunge wetu hata upige simu vipi hapokei.Tunaishi maisha ya shida sana,hapa hatuna umeme wanaohusika kila siku wanatupa majibu rahisi tu sasa tunaiomba Serikali itusaidie,”amesema Soloka.

 Vilevile,amesema wanakabiliwa na changamoto ya barabara kuwa mbovu katika eneo hilo hali ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu.

 “Huku kwetu ni makorongo mtindo mmoja,shida inakuja mama mjamzito akitaka kupelekwa Hospitali haiwezekani kwani gari haiwezi kufika,magari hayafiki huku kwetu hakuna barabara,”amesema Soloka.

 Alipotafutwa kwa njia ya simu  Mwenyekiti wa Kata hiyo,Mwahu Ibuma alisema kwamba yupo kwenye kikao na alipotafutwa kwa mara nyingine alidai yupo safarini.

 Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini,Ally Makoa (CCM) alipotafutwa kwa njia ya simu,simu yake iliita bila kupokelewa kwa zaidi ya mara 5.



Post a Comment

0 Comments