📌EZEKIEL
KAMWAGA
Imesadifu kwamba msiba wa kitaifa wa
hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu, utafanyika
katika jiji la Dodoma - ambalo kama isingekuwa uongozi wake pengine bado
usingekuwa na hadhi ulionayo leo.
Wakati Magufuli akiingia madarakani
mwaka 2015, hakuna aliyetaraji kuwa serikali nzima ingekuwa imehamia huko
katika kipindi cha miaka mitano yake ya kwanza tu madarakani.
Ingawa serikali ilifanya uamuzi wa
kufanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi mnamo mwaka 1973, jambo hilo -kwa
sababu tofauti tofauti, halikuweza kufanikiwa hadi Magufuli alipoonyesha kwamba
inawezekana tena ndani ya muda mfupi.
Wakati Watanzania na wananchi wa
Dodoma wakimuaga katika Uwanja wa Jamhuri mnamo Machi 22 mwaka huu - itakuwa ni
buriani kwa mwanasiasa ambaye kipekee kabisa alikuwa na maono na nguvu ya
kutekeleza alichokipanga, hata kama jambo hilo halilikubaliwa na wengi.
Danadana
za Dodoma kuwa makao makuu
Serikali iliamua kuifanya Dodoma
kuwa makao makuu kwa sababu moja kubwa - kwamba tofauti na Dar es Salaam iliyo
pembezoni Mashariki mwa nchi, yenyewe iko katikati ya nchi na hivyo ni rahisi
kufikika kwa watu wote.
Mpango wa serikali ulikuwa kwamba
mchakato huo wa kuhamia Dodoma uchukue muda wa miaka 10. Kwa maana hiyo,
serikali ilitakiwa iwe imehamia huko kufikia mwaka 1983.
Kampuni ya masuala ya mipango miji
ya PPAL kutoka Canada ndiyo ilipewa kazi ya kupanga namna mji huo utakavyokuwa
- wenye bustani za kutosha, njia za watembea kwa miguu, baiskeli na magari na
mbwembwe zingine. Kwa sababu Tanzania ilikuwa ikifuata sera za kijamaa wakati
huo, Dodoma pia ilitakiwa kuakisi itikadi hiyo katika kujengwa kwake.
Ingawa aliyekuwa Rais wa Tanzania
wakati huo, hayati Julius Nyerere, alikuwa na nia ya dhati ya kuhamia Dodoma,
matukio yaliyofuata baada ya uamuzi huo yalisababisha serikali isitimize
dhamira yake hiyo.
Katikati ya miaka ya 1970, dunia
iliingia katika mtikisiko wa uchumi uliosababisha hali ngumu na baadaye
Tanzania ikapata majanga ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
mwaka 1977 na Vita ya Kagera ya mwaka 1978/79 ndiyo ikazima kabisa ndoto hizo.
Wakati Ali Hassan Mwinyi alipoingia
madarakani mwaka 1986, uchumi wa Tanzania ulikuwa katika hali mbaya sana kiasi
kwamba isingewezekana kupata fedha za kutumia kwenye ujenzi wa mji mkuu mpya.
Kufikia mwaka 1993, mmoja wa wasomi
maarufu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi, Lusuga Kironde, aliandika
chapisho maarufu lililoeleza kwamba ingawa takribani dola milioni 4.9 (zaidi ya
shilingi bilioni 10 kwa viwango vya sasa) zilikuwa zimetumika kwenye mradi wa
kuhamia Dodoma, ilikuwa vigumu kwa ndoto hiyo kutimia.
Mwaka 2004, msomi mwingine
mashuhuri, Dk. Aloysius Mosha, kutoka Chuo Kikuu cha Gaborone nchini Botswana,
aliandika chapisho lililoonyesha kwamba jambo hilo ni kama limeshindika - labda
kama atapatikana mtu mwenye uwezo wa kulisukuma mbele.
Kila nikisikia kuhusu uamuzi wa
Magufuli kuhamishia serikali Dodoma, huwa nakumbuka tukio moja la mwaka 2017.
Nilikuwa mji mkuu kwenda kumsalimu
mmoja wa rafiki zangu ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa Naibu Waziri katika
Serikali ya Rais huyo wa Awamu ya Tano.
Nilipoingia ofisini kwake, sikuona
jambo lolote lililonionyesha kuwa niko ofisini kwa mtu wa wadhifa wake. Kaofisi
kalikuwa kadogo na watu wamebanana kwelikweli.
Wizara mbili tofauti zilikuwa zimehamishiwa
sehemu moja.
Kuna watumishi walikuwa wakilalamika
kwamba wamelazimishwa kuhamia Dodoma wakati mji wenyewe hauna maji, shule wala
huduma muhimu za kiwango cha juu katika maeneo kama afya na mengineyo. Sikuona
watu wenye furaha katika ofisi zile za serikali.
Lakini Magufuli alishikilia ajenda
hiyo na sasa, hata kama kuna minong'ono ya hapa na pale, watumishi wa serikali
wamekubali kuwa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi.
Huduma za muhimu zimeanza kuimarika
ikiwamo ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, shule kadhaa binafsi za
kimataifa zimeanza kujengwa Dodoma na bei za viwanja zimeanza kupanda.
Miaka mitatu iliyopita, mkoa huo
uliongoza kwa kukusanya kodi kubwa kuliko mikoa yote nchini na Magufuli
mwenyewe alimalizia ujenzi wa Ikulu ya Chamwino na katika siku zake za mwisho
madarakani alikuwa akikaa zaidi Dodoma kuliko Dar es Salaam.
Katika siku ya mwisho ya kampeni za
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Magufuli alishangaza wengi kwa uamuzi wake wa
kuamua kutumia siku hiyo kuzungumza na wazee wa mkoa wa Dodoma badala ya
kufanya mkutano wa hadhara kama ilivyozoeleka.
Huko nyuma, ilizoeleka kwa marais wa
Tanzania kuhutubia taifa kupitia mazungumzo na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam
lakini hatua ile ya Magufuli ilionyesha rasmi sasa kwamba mamlaka yamehamia
rasmi Dodoma na si kwa maneno pekee bali matendo.
Dodoma
itaendelea kung'ara baada ya Magufuli?
Wakati wananchi na viongozi
wakijiandaa kumuaga Magufuli, swali kubwa ambalo litakuwa vichwani mwa wengi ni
endapo uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, utaendeleza
alipoishia Magufuli au utarejea Dar es Salaam kulikozoeleka.
Kuna mambo makubwa ambayo Magufuli
aliahidi kwa watu wa Dodoma ambayo yanasubiriwa kwa hamu. Kwanza watu wanasubiri
kukamilika kwa reli ya mwendokasi (Standard Gauge) ambayo hatua yake ya pili
itaishia eneo la Makutupora.
Lingine ni ujenzi wa uwanja mkubwa
wa kisasa wa mpira wa miguu unaotarajiwa kutoa ajira nyingi kwa vijana wa mkoa
huo. Ni uwanja uliopangwa kuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji wengi kuliko ule
wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam.
Lakini bado Dodoma inahitaji ofisi
nyingi zaidi, majengo mengi zaidi, shule nyingi zaidi na huduma nyingi za
maendeleo.
Katika chapisho lile la Kironde,
alionyesha kwamba fedha nyingi zilizotumika katika awamu zilizopita ziliangalia
eneo la huduma pekee na si miundombinu.
Utawala wa Magufuli ulikuwa maarufu
kwa kuangalia miundombinu.
Watanzania wanamlilia Magufuli kwa
mengi, lakini wananchi wa Dodoma watamlilia zaidi kuliko wengine Tanzania -
labda wakizidiwa tu na watu wa mahali alikozaliwa; Chato.
Kwao, huu ni msiba wa Rais
aliyeupenda mkoa wao. Huu ni msiba wa Rais aliyewapenda watu wa Dodoma - akiwatania
kama watani zake kila alipopata fursa ya kufanya hivyo.
Kwao, huyu ndiye Rais aliyeuvunja
mfupa uliowashinda watangulizi wake wote wengine katika ofisi hiyo.
0 Comments