SIKU 10 ZATENGWA KUSHUGHULIKIA MIGOGORO YA ARDHI DODOMA

 


📌JACKLINE KUWANDA

OFISI ya Mkuu wa Mkoa Dodoma imetenga siku kumi (10) kwaajili ya kushughulikia migogoro ya Ardhi kwenye kata 41 na mitaa 226 ya jiji la Dodoma.

Zoezi hilo litashirikisha watalaamu wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi ,Ofisi ya Ardhi ya Mkoa ,Ofisi ya jiji la Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ofisini kwake,Mkuu wa Mkoa Antony Mtaka, amesema imeundwa timu ambayo itahusisha watu wote ikiwemo Maafisa Ardhi,Maafisa Mipango,Wanasheria,Afisa wa utoaji hati,Ofisi ya Baraza la Ardhi na Maafisa ambao uwepo wao kwenye timu hiyo watatoa majawabu ya moja kwa moja kwa wananchi ambao watawafikia.

Zoezi hilo litaanza Julai 5 siku ya jumatatu ,siku hizi (10) tumezigawanya katika siku tatu za mwanzo tarehe 5,6 na 7 zoezi hili litafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, tunawakaribisha wananchi wote wenye mamalamiko ya migorogoro ya Ardhi ,Maafisa wetu watakuwepo kusikiliza kero na kutolea majawabu 

Mtaka

Aidha,Mtaka amesema zoezi hilo litaendeshwa kwa njia ya tekinolojia akiwa na maana ya kuwa mwananchi anayehudumiwa kuazia Julai 5 hata kama viongozi aliyowakuta kwa siku ya kwanza hawapo atakapo kwenda kwenye Ofisi ya Serikali kuhusu suala la ardhi atashughulikiwa vizuri.

‘’kwa wananchi ambao hawawezi kufika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete tunazo siku saba ,tunayo timu ya wataalamu itaganywa kwenda kwenye kata 41 ili kuwafikia wananchi na kuweza kusikiliza kero zao,kusajili kero na zile zenye uwezo wa kutatuliwa zitatuliwe, kwahiyo kwa wanachi wanao kaa maeneo ya mbali hawana haja ya kuja pale kwasababu baada ya tarehe 7 julai timu yetu ya wataalamu itaenda kwenye maeneo yao kusaidia wananchi hao’’amesema Mtaka

Wakati huo huo ,Mtaka amewataka wananchi wa Dodoma kutumia fursa hiyo ya siku kumi (10) ili kupunguza shida za wananchi kutoka nyumbani kwenda kwenye Ofisi kwaajili ya kushughulikiwa migogoro hiyo.

‘’Niwaombe sana wananchi wa jiji la Dodoma kutumia siku hizi kumi (10) tuweze kusaidiana kutatua kero za wananchi kwenye migogoro ya Ardhi ,lengo letu sisi kama viongozi wa Mkoa na matarajio yetu ni kuona kuwa migogoro ya Ardhi inasikilizwa ,inapatiwa majawabu ,inamalizika ili kuwa na makao makuu ya nchi ambayo haitakuwa na migogoro hiyo, lakini kwa wanachi ambao wako nje ya dodoma na wana maeneo yao watumie siku hizi kumi kutenga muda wapate nafasi ya kuja’’amesema Mtaka

Katika hatua nyingine ,Mtaka amesema zoezi hilo litakapomalizika katika jiji la Dodoma litaenda katika Wilaya zilizopo Mkoani hapa.

Hata hivyo,Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kuwasisitiza wanachi kuwa kila mmoja mwenye mgogoro wa Ardhi anapaswa kwenda kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete ili Maafisa wanapokwenda kule wawakute na kushughulikiwa kero zao.

Post a Comment

0 Comments