DKT. GWAJIMA ATAKA KASI ZAIDI UANZISHWAJI MADAWATI YA JINSIA

 


📌WMJJWM


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametaka kuongezeka kasi katika uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu na kati kwani kumekuwa na kasi ndogo kuliko ilivyoelekezwa na Serikali.

Dkt  Gwajima amebainisha hilo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 23/03/2022.

Dkt.Gwajima amefafanua kwamba, Wizara iliandaa mwongozo na kuratibu uanzishwaji wa madawati haya kwa lengo la kuweka mfumo wa kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kingono na vitendo vya ukatili katika vyuo vya elimu ya juu na kati na kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto dhidi ya vitendo hivyo.

Katika vyuo hivi nimefuatilia takwimu, kasi ya uanzishwaji wa madawati haya ni ndogo sana, hivi vyuo vilitakiwa vione umuhimu wa uwepo wa madawati haya, nadhani kuwe na mawasiliano kati ya Baraza hili na mabaraza ya vyuo kuona sera ya usawa wa kijinsia katika vyuo inavyotekelezwa" amesisitiza
Dkt. Gwajima.

Waziri Gwajima ameoneshwa kusikitishwa pia na baadhi ya wafanyakazi wa vyuo kuwa vikwazo vya uanzishwaji wa madawati hayo kwa wao wenyewe kufanya unyanyasaji wa kijinsia.

Ameongeza pia Serikali itahakikisha mwongozo huo unafika hadi katika shule za Msingi na Sekondari ili kusaidia mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Aidha,Dkt. Gwajima amesema, Dunia yote kwa sasa inaelekea kwenye kuimarisha usawa wa kijinsia hasa kwenye masuala ya kiuchumi hivyo ametoa wito watanzania kujipanga kupata fursa hizo kupitia Kamati iliyoundwa kuratibu utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la usawa wa kijinsia.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara  Dkt. Zainab Chaula, amemuhakikishia Waziri kuwa Wizara itaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ili kutokomeza vitendo vya ukatili kwani ndiyo msingi katika kuimarisha usawa wa kijinsia.

Dkt. Chaula amesema pamoja na changamoto zilizopo, Wizara imejipanga kushughulikia Ustawi na Maendeleo ya jamii kwa makundi yote kwani ndiyo chachu katika maendeleo ya Taifa.

Suala la ukatili wa kijinsia tumelishikia bango japo bado halijaongelewa vya kutosha, tutaendelea kwa kushirikiana na wadau. Vilevile kuhakikisha tunatatua changamoto ya uhaba wa watumishi, ukosefu wa ajira na uchakavu wa majengo hasa ya makazi ya wazee
Dkt. Chaula.

Dkt. Chaula ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua umuhimu wa usawa wa kijinsia na kuchagua kuwa kinara katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE katika Wizara hiyo Ikusubisya Kasebele ameshukuru uongozi wa Baraza hilo kwa kufuata sheria na kukaa kikao mara mbili kwa mwaka na kuhusisha wajumbe kutoka maeneo yote yanayosimamiwa na Wizara hiyo.

Kasebele ameongeza kuwa wajumbe wote wana haki ya kuchangia mawazo yao ikiwemo kupitia bajeti iliyoandaliwa kwa maslahi ya Taifa.

 

 

Post a Comment

0 Comments