MIFUMO YA TEHAMA YAANZA KUPIMA UTENDAJI KAZI SERIKALINI

 

📌RHODA SIMBA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama wamebainisha utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kutumia mifumo ya TEHAMA katika kupima utendaji kazi Serikalini ili kuimarisha uwajibikaji na utoaji huduma bora.

Wakiongea Jijini Dodoma wakati wa mkutano na Viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuhusu mtazamo wa Serikali ya awamu ya sita katika uimarishaji wa Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma bora kwa Utumishi wa Umma, wamesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho ya kisekta na mtambuka ya kujenga mifumo ya TEHAMA.

Pamoja na juhudi za Serikali za kupima utendaji kazi Rais ameelekeza ushirikishwaji wa vyama vya wafanyakazi na amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuendelea kuwa daraja kati ya waajiri na wafanyakazi kwa kuchochea na kuhimiza utamaduni wa kudai haki na kutimiza wajibu wao,

Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu imeendelea kutekeleza maagizo ya Mhe, Rais kwa kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji wa Vibali vya Kazi kwa raia wa kigeni. Mfumo huo umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku za kazi 14 hadi siku 7. Aidha, Mfumo huo umeimarisha uwazi na uwajibikaji

Ndalichako

Nae Mhagama amesema kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetekeleza maagizo ya Rais kwa kujenga na kufanya maboresho katika mifumo ya Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS), Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi (PIPMIS).

Mifumo mingine ambayo imetekelezwa na Ofisi hiyo kuwa ni; Mfumo wa e-mrejesho, Mfumo maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu, Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal) pamoja na mfumo wa SEMA NA WAZIRI

Mhagama

Katika hatua nyingine, Mhe. Mhagama amesisitiza kuwa utekelezaji wa maagizo hayo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Dira na maono yake yanakamilika ambapo anapenda kuwa na Utumishi wa Umma unaofanya kazi kwa: Uadilifu; Uwajibikaji; Bidii na Weledi; Haki na Uzalendo wa Kitaifa.

Kadhalika mewataka Viongozi wa Wafanyakazi pamoja na kusimamia haki na maslahi ya Watumishi wa Umma kuhakikisha wanawasimamia Watumishi wa Umma ili kuhakikisha wanachapa kazi kwa utalaam, ubunifu, weledi wa hali ya juu na kwa kuzingatia maadili ya utendaji katika Utumishi wa Umma ili kufikia dira, maono na azma ya kiongozi Mkuu wa Nchi.


Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT)Deus Seif amesema wao kama vongozi wa vyama vya wafanyakazi wamewapongeza Mawaziri hao na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Kwa kujenga mifumo ya TEHAMA, inayoimarisha Utumishi wa Umma na uwajibikaji wa hiyari.

Nataka kusema tu kuwa hali hiyo imeonesha dhamira ya dhati kabisa ya Serikali kuwajali wafanyakazi nchini na sisi kama viongozi wa vyama hivi vya wafanyakazi tunaenda kusimamia na kutekeleza maagizo haya ambayo tumepewa leo na mawaziri wetu

Seif.

 

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments