WAKUNGA WATAKIWA KUONGEZA KUJITUMA, KUFANYA KAZI KWA UANGALIFU



📌RHODA SIMBA

SERIKALI imewataka wakunga wote nchini kufanya kazi kwa uangalifu, weledi, uaminifu, kujituma na kufuata maadili ya taaluma yao kwani kuna baadhi wamekuwa wakikiuka misingi ya kazi hiyo.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Abel Makubi wakati akifungua kongamano la kisayansi la wakunga kuelekea maadhimisho ya siku ya ya wakunga duniani kwa niaba ya Waziri wa Afya ambapo amesema kuwa kuna baadhi ya wanataaluma wachache huwa wanaharibia wengine kwa kukiuka maadili na kusababisha madhara kwa wapokea huduma.

"Naagiza Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kushirikiana na idara pamoja na baraza wajielekeze katika kuweka mifumo ya kuimarisha maadili na kujengea uwezo wakunga kuwa waadilifu na kwa wale wanaoenda nje ya mstari basi baraza lifanye kazi yake ya kuwarudisha kwenye mstari,"amesema Makubi

Aidha Makubi amesema kuwa takwimu za utafiti wa afya zinaonesha kuwa pamoja na uboreshaji unaofanyika katika sekta ya afya lakini bado kuna wajawazito ambao hawajifungulii katika vituo vya kutolea huduma. 

Amesema kuwa baadhi ya sababu zinazowafanya wajawazito kutojifungulia katika vituo vya huduma ni pamoja na kuchelewa kupata huduma pamoja na kauli za watoa huduma kutokuwa rafiki.

"Pamoja na kuwa kumekuwa na ongezeko la wakina mama kujifungulia katika vituo vya huduma lakini takwimu zimeonesha ongeko la vifo vya wanawake wajawazito kutoka 432 ( Sensa 2012 ) hadi kufikia vifo 556 (TDH 2015/16) kwa kila vizazi hai100,000,

Hii inamanisha kuwa wakina mama 30 wanakufa kila siku na 11,000 wanakufa kila mwaka na wengi wanafia katika vituo vya kutolea huduma. hali hii haikubaliki kabisa,"amefafanua.

Kadhalika amesema kuwa utafiti wa afya wa mwaka 2015/16 umeonyesha kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 81 hadi vifo 67 kwa watoto chini ya miaka mitano, vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kutoka 51 hadi 43.

Aidha amesema kwa upande wa vifo vya watoto wachanga bado kumekuwa na changamoto ambapo vimeshuka kwa kiwango kidogo cha kutoka 26 hadi 25 tu kwa kila vizazi hai 1000.

 "Ili kuweza kupambana na vifo vya watoto wachanga Serikali itaendelea kuimarisha miundo mbinu ya huduma kwa vichanga yani Neonatal Intensive Care Units (NICU) sambamba na upatikanaji wa ujuzi wa kutosha kwa wakunga,"amesema.

Nichukue nafasi hii pia kukishukuru Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kwa maandalizi ya siku hii na kunialika kuwa mgeni rasmi katika kufungua kongamano hili la kisayansi la siku 3 kuelekea maadhimisho ya wakunga Duniani.

 Kwa upande wake muwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mary Shadrack ameainisha sababu zinazopelekea vifo kwa mama na mtoto huku mkurugenzi msaidizi afya ya uzazi na mtoto kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Mahuwani akitaja mambo muhumu yakuzingatia ili kupunguza ama kumaliza vifo kwa mama na mtoto kuwa ni kusimamia na kuwajengea uwezo wakunga wanaotoka vyuoni, kuwajengea uwezo wakufunzi wakunga kwakutoa elimu kwa vitendo na kuboresha mazingira ya kazi kwa wakunga.

Awali akizungumzia kuhusu kongamano hilo rais wa Chama Cha  Wakunga tanzania (TAMA) Feddy Mwanga ameeleza umuhimu wa kongamano.

"Siku hii siyo muhimu kwa wakunga tu, bali kwa jamii na Taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa ya kutathmini kazi za Ukunga na kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha ubora wa huduma hasa kwa akina mama na Watoto,Hivyo kwa pamoja tunaungana na Wakunga duniani kote kuwapongeza katika kuadhimisha siku hii muhimu huku Kauli Mbiu ya Mwaka huu ikiwa ni “Invest in Midwives: Save lives ” kwa maana ya “Wekeza kwa Mkunga: Okoa Maisha”.amesema Mwanga

Siku ya Wakunga huadhimishwa duniani kote tarehe 5 mwezi Mei ya kila mwaka kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na wakunga pamoja na kuwahamasisha wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa huduma bora kwa akina mama na watoto ambapo maadhimisho haya kwa mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo "ajenda 2030 tokomeza vifo vitokanavyo na uzazi wekeza kwa mkunga mtaalam"

 

Post a Comment

0 Comments