BODI YA NYAMA: KILO HAMSINI YA NYAMA KULIWA NA MTU MMOJA KWA MWAKA.

 📌RHODA SIMBA

IMEELEZWA kuwa ili mwili wa binadamu upate virutubisho vyote muhimu mtu mmoja anatakiwa kwa wiki walau ale kilo moja ya nyama kwani virutubisho vinavyopatikana kwenye nyama nyekundu havipatikani kwenye mimea na kitaalamu mtu anapaswa kula nyama angalau kilo hamsini kwa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 28  kuhusu utekelezaji wa majukumu ya bodi ya nyama Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022-2023 msajili wa bodi hiyo Dkt. Daniel Mushi amesema kuna watu wamekuwa wakisema nyama ni mbaya lakini uzuri au ubaya wa kula nyama unatokana na kiasi cha nyama mtu anachokula na aina ya nyama anayokula.

Sisi kama Bodi ya nyama tunalo jukumu na mkakati wa kuwahamasisha watanzania wale nyama, niseme wazi hapa kuna mkanganyiko kidogo kuna watu wamesema nyama ni mbaya lakini suala la nyama kuwa mbaya au nzuri ni suala la kiasi cha nyama unachokula na aina gani ya nyama unakula

Dk Mushi

Aidha amesema kuwa endapo mtu atakula nyama kwa kiwango kinachotakiwa mtu huyo atakua na afya kwani itasaidia kuimarisha kinga ya mwili ya kupambana na magonjwa nyemelezi na nguvu ya kufanya kazi hivyo itasaidia kuongeza uzalishaji.

Kama mnavyo fahamu nyama ndio njia rahisi ya kuondokana na utapia mlo, mtu anapowaambia watanzania wasile nyama nadhani haelewi vizuri hali ilivyo katika ulaji wa nyama na sisi kama Serikali tunao mpango wa kuhamasisha watanzania wale nyama lakini ulaji nyama uliosahihi

Katika hatua nyingine amesema kuwa bodi itahakikisha inalinda afya ya mlaji kupitia udhibiti na ukaguzi sambamba na kuhamasisha uzajishaji bora wa nyama ili kupata masoko nje ya nchi.

Kwasasa mtanzania mmoja anakula nyama takribani kilo 15 kwa mwaka kuanzia Januari mpaka Disemba lakini tunapaswa kula nyama angalau kilo 50 kwa mwaka, kwa wenzetu Ulaya wanakula mpaka kilo 100 mtu mmoja kwa mwaka 
Sasa unapokula nyama kiasi kinachotakiwa kwanza unakuwa na afya unakuwa na nguvu ya kufanya kazi na uzalishaji unaongezeka lakini pia unakuwa na uwezo wa kinga ya mwili kuweza kujikinga na magonjwa kinga zinakuwa imara

Mwaka 2006 serikali ilitunga sheria ya tasnia ya nyama sura ya 421 yenye lengo la kuwezesha mabadiliko katika tasnia ya nyama, kuanzisha misingi thabiti ya usimamizi, kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora za nyama, kuendeleza ukuaji wa tasnia ya nyama na bodi ya nyama Tanzania ilianzishwa katika sheria hii ili kusimamia utekelezaji wa sheria husika.

 

Post a Comment

0 Comments