WAZIRI MKUU AAGIZA JIJI LA DODOMA, LATRA KUKUTANA KUBORESHA MACHINGA COMPLEX

 


📌MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma ukutane na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) ili kutengeneza mpangilio wa safari za daladala ndani ya jiji hilo kuelekea soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko barabara ya Bahi. 

Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi Novemba 24, 2022) mara baada ya kutembelea na kukagua soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko eneo la Bahi Road jijini Dodoma.

Majaliwa amesema sambamba na utekelezaji wa maagizo hayo Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Dodoma wanatakiwa kuhakikisha wanafanya maboresho ya stendi ili iweze kukidhi viwango vya kupokea magari ya abiria yatakayoelekezwa eneo hilo kwa kuboresha barabara inayopita nyumba ya soko ili kuimarisha njia za usafiri.

Pia, ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma isimamie utoaji wa fedha za mikopo kwa wafanyabiashara walioko katika soko hilo ili waongeze mitaji na kukuza biasharazao.   “Nataka nipongeze uamuzi wenu (wafanyabiashara wadogo) wa kuja hapa mmefanya maamuzi sahihi na mtanufaika.” amesema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amesema kuwa ni dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuwainua wafanyabiashara wadogo kwa kufungua milango ya ufanyaji biashara kwa uwazi na Serikali kuwapa huduma muhimu zitakazowasaidia kuleta tija kwenye shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha anafanyia kazi changamoto zilizojitokeza baada ya wafanyabiashara wadogo wadogo kuhamia katika eneo hilo ikiwemo kuweka vikingia mvua na kwa kushirikiana na TARURA kuweka taa za barabarani.

Awali akijibu maombi ya wafanyabiashara hao, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema Halmashauri ya Jiji imetenga Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara walioko sokoni hapo na hadi kufikia mwezi Disemba mwaka huu watakuwa wameshakamilisha taratibu za utoaji wa mikopo hiyo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Festo Dugange amesema ujenzi wa soko hilo ni dhamira njema ya Rais Samia Sulluhu Hassan ya kuwajali na kuwapenda wafanyabiashara wadogo wadogo ili waondokane na adha ya kutembea na bidhaa zao badala yake wapate sehemu nzuri na bora ya kufanya biashara zao.

Post a Comment

0 Comments