📌BAHATI MSANJILA
Afisa Mtendaji Mkuu
wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na
Serikali kwa kutumia majukwaa yake kuhakikisha huduma mbalimbali zinazotolewa
na taasisi za umma zinawafikia wananchi kwa urahisi, ufanisi na ubora
unaotakiwa.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam mbele ya maafisa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waliokuwa
katika ziara ya mafunzo ya siku mbili ndani ya benki hiyo, Zaipuna alieleza
kuwa NMB imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ya kisasa inayowezesha
utoaji wa huduma bora kwa wateja, pamoja na kubuni suluhisho mbalimbali kwa
changamoto za kijamii.
Mbali na teknolojia,
benki hiyo pia imejikita katika utawala bora na kuwajengea uwezo wafanyakazi
wake ili kuhakikisha kila huduma inayotolewa inakidhi viwango vya juu vya
kitaalamu. Kupitia ushirikiano kati ya taasisi binafsi na serikali, NMB
inaamini changamoto nyingi za wananchi zinaweza kutatuliwa kwa pamoja kwa
haraka na ufanisi zaidi.
Kwa upande wao,
maafisa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria walieleza kuwa ziara yao imelenga
kujifunza namna bora ya kuboresha kituo cha huduma kwa wateja walichokianzisha
mwaka jana, ambacho kinapokea malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi kupitia
simu na mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa wizara
hiyo, lengo la kituo hicho ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake kwa
wakati ili kujenga jamii tulivu, inayoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli
za kiuchumi, na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na
taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo,
maafisa hao walitembelea vitengo mbalimbali vya huduma kwa wateja ndani ya
benki hiyo na kujionea namna teknolojia inavyotumika kuboresha huduma, jambo
lililowapa mafunzo ya moja kwa moja yatakayosaidia katika maboresho ya huduma
za wizara yao.
0 Comments