WADAU WA AFYA WATAKIWA KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA USUGU WA VIMELEA VYA DAWA.



📌NA DOTTO KWILASA
WADAU  wa afya nchini wametakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya tatizo la usugu wa vimelea vya dawa kwa kuongeza uelewa kwenye jamii na kutia hamasa kuhusu usugu wa dawa za binadamu ambao  unatishia afya za binadamu  duniani kote.

Hayo yamelezwa jana jijini hapa na Mtendaji Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la kupambana na tatizo la usugu wa vimelea vya dawa (RBA-INITIATIVE) Erick Venant katika mahojiano maalumu blog hii jijini Dodoma.
Akieleza zaidi amesema,licha ya juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema bado kuna baadhi ya watoa huduma za afya nchini hawazingatii taratibu za kitabibu katika kutibu wagonjwa kwa kuwapatia dawa bila utaratibu maalumu.

Kuna umuhimu wa elimu zaidi kutolewa kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu usugu wa dawa za binadamu unaotokana na utolewaji wa dawa kiholela bila cheti cha daktari na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu
Eric Venant


Aidha  amebainisha baadhi ya sababu zinazochangia usugu wa dawa kwa binadamu kuwa ni pamoja na kutumia dawa bila kupima na kupata ushauri  wa kitabibu,kutokukamilisha dozi pamoja na matumizi ya dawa za binadamu kwa mifugo .

Kutokana na hayo Venant ametoa ushauri kwa  wadau wa afya hususani wafamasia kuwa na utaratibu wa kutoa huduma baada ya kupokea cheti kutoka kwa Daktari ili kunusuru afya za wateja wao.
Erick Venant baada ya kupokea tuzo ya Legacy jijini London mwaka 2019.Erick alipewa tuzo hiyo kutambua mchango wake katika kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa(Antimicrobia Resistance)

Aidha Mtendaji Mkuu huyo ambaye kitaaluma ni Mfamasia,amesema RBA-INITIATIVE kama wadau wa kupambana na tatizo la usugu wa vimelea vinavyosababishwa na matumizi mabaya ya dawa  wanaanda mpango mkakati ambao Utasaidia kutokomeza usugu wa dawa ili kulinda maslahi ya watanzania kwa ujumla.

Amesema,kwa kuzingatia umuhimu wa afya ya watanzania shirika hilo litafanya kampeni ya kukomesha usugu wa dawa kwa jamii yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu usugu wa dawa za binadamu.

Baada ya kukamilisha taratibu zote ,tutaanza kutoa elimu kwa jamii namna ya kuepukana na tatizo la usugu wa dawa kwa kusisitiza zaidi matumizi sahihi ya dawa yanayotolewa na wataalamu ambapo kwa kuanza tutaanza   kuzifikia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwani tunaamini ni mabalozi wazuri.
Erick Venant.

Hata hivyo ameiomba  mamlaka ya usimaminzi wa chakula na dawa (TMDA) kuhakikisha wanayafungia maduka yote ya dawa ambayo yanaendelea kukiuka taratibu za kifamasia .

“Lazima tuwe na huruma kwa binadamu wenzetu,ikiwa sheria na miongozo ya kiafya itafuatwa itasaidia wafamasia  kufanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na utekelezaji  wa sheria za afya”amesema.

Pia ameeleza kuwa  Usugu wa dawa ni hali ya dawa kushindwa kuua vimelea vya magonjwa  au kuzuia ukuaji wake na hivyo dawa kushindwa kudhibiti vimelea hivyo.

Napenda kuikumbusha jamii kuwa  vimelea vya magonjwa ndio hujenga usugu wa dawa,jamii inapaswa kupiga Vita matumizi mabaya ya dawa
Erick Venant

Post a Comment

0 Comments