📌DOTTO KWILASA
SERIKALI imewataka wataalamu wanaofanya tathimini ya
uhakika wa usalama wa chakula na lishe kufanya tathmini hizo kwa
kuzingatia mazingira husika kwa kuangalia mitazamo ya ndani ya nchi badala ya
kutumia mifumo ya nje ambayo wakati mwingine hukosa uhalisia wa maisha ya
watanzania.
Hayo yamesemwa Jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
kilimo, Prof. Siza Tumbo wakati akizindua Mfumo wa Uchambuzi wa Uhakika wa
Chakula na Lishe Tanzania (MUCHALI) unaoratibiwa na Shirika la kilimo na
chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo
nchini.
Prof.Tumbo amesema, hali ya kufanya tathmini ya chakula
nchini bado hairishishi kwani mara nyingi wataalamu hutumia mbinu za kutoka nje
na kuzitumia katika kufanya tathmini za ndani ya nchi jambo ambalo linatakiwa
kufanyiwa marekebisho.
Tafiti nyingi za masuala ya chakula na lishe hazijaleta mafanikio kwa sababu Mara nyingi wataalamu wetu hawazingatii uhalisia wa maisha ya watanzania yalivyo,nawaomba mnapofanya tafiti,tafiti zenu ziendane na mazingira husika
Mbali na hayo Naibu Katibu mkuu huyo ametumia nafasi hiyo kuwataka watanzania kuzingatia ulaji wa vyakula vya asili vinavyojenga na kuongeza kinga ya mwili hali itakayoimarisha afya badala ya kutumia vyakula vya kisasa ambavyo asilimia kubwa huchangia udhaifu wa kinga ya mwili .
Amesemà ,nchini Tanzania maeneo yote yamezungukwa na vyakula vya
asili hivyo ni wajibu kuvitumia ili kukabiliana na maradhi mbalimbali ambayo
wakati mwingine hutokana na ulaji wa vyakula vilivyosindikwa usio na
mpangilio .
Kwa umuhimu huo,amewataka wataalamu hao wa mfumo wa uchambuzi wa
chakula na lishe kujiendesha kidijitali ili kuweza kuwa sehemu ya dunia.
Dunia ikiwa katika Mfumo wa digitali hatuna pa kujifisha,hatua hii ya MUCHALI inapaswa kuendeshwa kisasa zaidi ili kuwa na nguvu ya pamoja
Naye Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la
Mpango wa Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO),Stella Kimambo
amesema muongozo uliozinduliwa utatathmini hali ya chakula na lishe kwa ngazi
ya mkoa na wilaya .
Mbali na hayo ameainisha hatua muhimu ambazo zitachukuliwa
na MUCHALI Kupitia wadau wengine wakati wa ukusanyaji kuwa ni pamoja
na uchambuzi na usambazaji wa taarifa za usalama wa chakula ili jamii
ipate mwamko na kuwa na matumizi sahihi ya lishe .
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhakika wa Chakula na Lishe kutoka
Zanzibar,Hamad Masoud Ali amesema kuwa amefurahishwa na mwenendo mzima wa
MUCHALI huku akisisitiza kuwa hatua hiyo inapaswa kuendeshwa kidijitali ili
kufanikiwa.
Kutokana na hayo ameahidi kufanya mabadiliko ya muongozo wa tathmini ya usalama wa chakula na lishe kwa upande wa Zanzibar kwa kuzingatia mabadiliko ya kisera ikiwemo muundo wa serikali za mitaa ambao awali haukuwepo ili kufanikisha zoezi hilo.
0 Comments