KAYA MASIKINI ZANUFAIKA NA TASAF, SERIKALI YAJINADI MAFANIKIO YA MIAKA MINNE

 



📌BAHATI MSANJILA


Kaya zaidi ya milioni moja masikini zinaendelea kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), mpango ambao Serikali ya Awamu ya Sita inautekeleza kwa mafanikio makubwa kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, anawasilisha taarifa hiyo jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya utumishi wa umma na utawala bora kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Amebainishaa kuwa ruzuku ya TASAF imewasaidia walengwa kuboresha maisha yao kwa kugharamia elimu ya watoto, kupata huduma za afya, kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato na kuboresha makazi, hivyo kupunguza kiwango cha umaskini, hasa vijijini.

 

Waziri Simbachawene ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusimamia ipasavyo mpango huu ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa, na kwamba hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo jumuishi.

 

Katika hotuba yake, ametaja pia mafanikio katika sekta ya ajira na usimamizi wa watumishi wa umma, ambapo zaidi ya watumishi 133,317 wameajiriwa katika kipindi cha miaka minne. Kati yao, ajira 55,162 zinatolewa kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

 

Amesema ajira nyingi zinatolewa kwa kada za elimu, afya na kilimo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo.

 

Ameongeza kuwa kiwango cha utoaji wa ajira kimeongezeka kwa asilimia 163.19 kutoka mwaka 2020 hadi 2024.

 

Katika kuboresha mazingira ya kazi, Serikali inapandisha vyeo watumishi 610,733 na kubadilisha kada za watumishi 42,515, huku ikiendelea kuondoa tozo zisizo na tija kwa watumishi wakiwemo waliokopa mikopo ya elimu ya juu. 

 

Pia, kiwango cha chini cha kodi ya mapato (PAYE) kinapunguzwa kutoka asilimia 9 hadi 8 ili kuongeza kipato kwa mtumishi.

 

Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali inaboresha mifumo ya uwajibikaji kwa kuimarisha kamati za uadilifu, ambapo hadi sasa Kamati 59 zenye wajumbe 700 zinapatiwa mafunzo ya maadili. 

 

Aidha, mfumo wa e-Mrejesho unaotumika kupokea hoja za wananchi unapokea maoni, malalamiko na mapendekezo ambapo hoja zaidi ya 146,204 zimepokelewa na asilimia 99 ya hoja hizo zimeshapatiwa majibu.

 

Katika kuhakikisha utawala bora unaimarika, Serikali inakamilisha mfumo wa kidigitali wa kushughulikia rufaa za watumishi, inafanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria katika taasisi 543, na inasisitiza uadilifu, weledi na uwajibikaji kwa watumishi wake wote.

 

Aidha amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, jambo linalodhihirishwa na ripoti ya Taasisi ya Transparency International ya mwaka 2024, iliyotolewa rasmi Februari 11, 2025.

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepata alama 41 na kushika nafasi ya 82 kati ya nchi 180 duniani, ikiwa ni ongezeko la alama moja na kupanda nafasi tano kutoka alama 40 na nafasi ya 87 mwaka 2023.

 

Simbachawene amesema mafanikio hayo ni kielelezo cha juhudi madhubuti zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha utawala bora na uwajibikaji vinatawala nchini.



 






Post a Comment

0 Comments