📌BAHATI MSANJILA
Benki ya NMB inaendelea kuonesha dhamira yake ya
kuwekeza kwenye michezo na maendeleo ya vipaji nchini baada ya kukabidhi vifaa
vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 19 kwa timu za Mashujaa kutoka
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imefanyika katika
makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na viongozi wa NMB
pamoja na wawakilishi kutoka JWTZ.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kusaidia timu za
Mashujaa Queen na Mashujaa Under 20 katika maandalizi ya michezo yao
mbalimbali.
Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi kutoka NMB,
Ally Ngingite, amesema benki hiyo imekuwa na uhusiano mzuri na JWTZ kwa muda
mrefu, hasa kwenye sekta ya michezo.
Amesisitiza kuwa NMB inatambua mchango wa jeshi
hilo katika kukuza vipaji na kuimarisha michezo, jambo linaloleta mshikamano,
afya bora na maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utimamu wa Mwili,
Michezo na Utamaduni kutoka JWTZ, Kanal David Luoga, ametoa shukrani kwa NMB
kwa kuwa mdau wa kuaminika katika kukuza michezo ndani ya jeshi.
Ameeleza kuwa michezo ni njia mojawapo ya
kudumisha furaha, mshikamano na afya kwa wanajeshi na jamii kwa ujumla.
Katika vifaa vilivyokabidhiwa, kuna jezi za
kuchezea seti nne, gloves za magolikipa seti nne, track suit hamsini, jezi za
kusafiria arobaini pamoja na sanamu za mazoezi. Vifaa hivi vitasaidia si tu
kuinua morali ya wachezaji, bali pia kuongeza ubora wa maandalizi yao kuelekea
mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Kupitia mchango huu, NMB inaendelea kujikita
katika kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii, huku ikitanguliza maendeleo ya
vijana na vipaji kama sehemu ya mkakati wake wa uwajibikaji kwa jamii.
0 Comments